MENU

Where the world comes to study the Bible

Somo 5: Dhambi Na Wokovu

Related Media

“Tunaamini kwamba wokovu ni zawadi ya Mungu na mwanadamu huipokea kwa imani binafsi katika Yesu Kristo na kujitoa ili kusamehewa dhambi. Tunaamini kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa neema kwa imani na si kwa matendo (Matendo 13:38-39, Warumi 6:23, Waefeso 2:8-10). Tunaamini kwamba waamini wote wa kweli, wakishaokolewa, huhifadhiwa salama milele (Warumi 8:1, 38-39; Yohana 10:27-30).”

Wokovu ni neno rahisi ambalo linajumuisha dhana nyingi—dhana ambazo haziwezi kueleweka kikamilifu kwa akili ya kawaida. Je, wokovu ni kwa ajili tu ya kuikimbia jehanamu? Je, ni bima ya maisha? Je, ni jambo ambalo Mungu alihitaji kulifikiria wakati Adamu na Hawa walipomwasi? La hasha, Maandiko yanatufundisha kwamba mungu aliupanga wokovu wetu kabla ya msingi wa ulimwengu, kwa sababu kwa kuwa anajua mambo yote, alijua kwamba mwanadamu atauhitaji sana.

Hitaji la Mwanadamu

  1. Kifo cha Kiroho-kutengwa na Mungu (walijificha na waliogopa)
  2. Kifo cha kimwili
  3. Asili ya dhambi iliyorithiwa na wazao wao wote.

Asili ya mwanadamu iliharibika au kupoteza thamani:

Fikra: 2 Wakorintho 4:4, Warumi 1:28
Maamuzi: Warumi 1:28
Dhamiri: 1 Timotheo 4:2
Moyo: Waefeso 4:18
Hali nzima ya mtu: Warumi 1:18-3:20

“Hali nzima ya mtu ina maana kwamba uharibifu wa dhambi unaenezwa kwa watu wote na inaenea katika maeneo yote kiasi kwamba hakuna kitu katika mwanadamu wa kawaida ambacho kinaweza kumfanya akubalike mbele za macho ya Mungu.” –Charles Ryrie

Mapaji ya Mungu

Ahadi na Picha

Kwa karne zote ambazo Agano la Kale lilipitia Mungu alitoa ahadi na mifano au picha za Mwokozi ambaye atamtoa baadaye kwa ajili ya wokovu wetu. Ahadi ya kwanza ilikuwa ni Mbegu ya mwanamke, ambaye Shetani angemjeruhi lakini mbegu hiyo baadaye ingemwangamiza shetani (Mwanzo 3:15).

Kisha aliwapa picha ya jambo ambalo Mwokozi angelifanya. Mwanzo 3:21: kila mnyama aliyetolewa sadaka katika Agano la Kale alimlenga Yesu Kristo. Kila madhabahu iliulenga msalaba.

Kutimilika kwa Kristo

Yesu Kristo ambaye ni Mungu-Mwanadamu, alikuwa ni Mungu katika mwili wa kibinadamu, ili aweze kuishi maisha yasiyokuwa na dhambi, akamwaga damu yake kwa ajili ya dhambi za watu wote, akafufuka kutoka kwa wafu na kisha kurudi mbinguni kuwa Mwombezi wetu.

Mambo yaliyokamilishwa na Kifo cha Kristo

Mbadala

Kuwa Mbadala ni maana kuu ya Kifo cha Kristo

Anti kwa kiyunani ina maana ya “kukaa badala ya” (Mathayo 20:28, Marko 10:45)

Huper ina maana ya “Kwa faida ya” au “kwa nafasi ya” (2 Wakorintho 5:21, 1 Petro 3:18). Yesu alikuwa Mbadala wetu kwa kuwa alikufa kwa ajili yetu. Alikuwa anatuwakilisha alipowambwa pale msalabani.

Mungu aliupenda ulimwengu kwa upendo ambao unaweza kupimwa kwa uwezo wake usiopimika wa kupenda. Mungu anawapenda viumbe wake kiasi kwamba anatutaka tuunganishwe naye. Alituumba ili tuwe na ushirika Naye. Lakini ushirika huo unashindikana kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu. Adhabu yake ni kifo cha kiroho na cha kimwili. Mungu ndiye Mwamuzi aliyeitangaza hiyo adhabu. Tabia ya Mungu ni kwamba hawezi kutenda bila haki yote. Mwanadamu akiwa katika hukumu ya kifo, hana anachoweza kufanya kwa juhudi zake mwenyewe ili kuiepuka hiyo hukumu ya kifo. Kwa hiyo Mungu mwenyewe alikuja kuichukua hiyo adhabu kwa ajili ya mwanadamu wa kiume na wa kike aliyempenda. Yesu Kristo alikuja kwa hiari yake kufa kwa niaba yetu, kwa dhambi zetu na kwa faida yetu. Alichukua adhabu kamilifu kwa ajili ya kifo cha kimwili na kiroho.

Ni kwa nini yeye alikuwa ndiye mbadala mkamilifu?

Mwanadamu—angeweza kufa kwa ajili ya mwanadamu: mwenye thamani ileile, lakini sio kama ya wanyama.

Asiye na dhambi—aliweza kufa kwa ajili ya dhambi, lakini sio dhambi zake.

Mungu asiyepimika—aliweza kufa kwa ajili ya dhambi zisizohesabika.

Je, hii ina maana gani kwangu na kwako? Kama nadaiwa dola 100,000 na sina kitu cha kulipa, na mtu mwingine akanilipia deni langu, mimi sihitaji kulipa tena. Ninakuwa sina deni tena. Kwa kuwa Yesu alinilipia adhabu kwa ajili ya dhambi zangu, sina haja ya kulipia tena adhabu hiyo—kama nikimpokea kama Mbadala wangu na kuachana na mawazo ya kufanya matendo mema ili niweze kukubalika na Mungu.

Ukombozi

Agorazo: Ina maana ya kununua au kulipa bei ya kitu.

Ina maana ya kulipa kile ambacho dhambi yetu ilidai ili sisi tuweze kukombolewa (I Petro 2:1, walimu wa uongo; 1 Wakorintho 6:20, 7:23; Ufunuo 5:9).

Exagorazo: Ina maana ya kununua kutoka sokoni

Wagalatia 3:13, 4:5: Kifo cha Kristo sio tu kwamba kililipa gharama ya dhambi lakini pia kilituondoa kwenye soko la dhambi ili kutupa uhakika kamili kwamba hatutarudishwa tena kwenye utumwa wa dhambi. Hatutauzwa tena kama watumwa wa dhambi.

Lutroo: Kufungua-kuweka huru

Tito 2:14, I Petro 1:18: Ni kuachiliwa na kuwekwa huru katika hali nzima ya kulipiwa. Mafundisho juu ya ukombozi yana maana ya kwamba kwa kumwagwa damu ya Kristo, waamini wamenunuliwa, wametolewa kutoka katika utumwa na kukombolewa.

Je, hii ina maana gani kwangu na kwako leo? Wewe na mimi tumewekwa huru kutoka katika mambo yetu ya zamani, kutoka katika utumwa wa bwana wetu wa zamani, Shetani, kutoka katika namna zetu za dhambi tulizoishi kwazo. Bei iliyolipwa kwa ajili yetu ilinunua uhuru wetu milele kutoka katika soko la watumwa na kamwe hatutakuwa tena jinsi tulivyokuwa zamani. Uhuru huu ndio urithi wangu katika Kristo.

Upatanisho

Kupatanisha ina maana ya kubadilisha kutoka hali ya uadui kwenda kwenye urafiki. Upatanisho kwa njia ya mauti ya Kristo ina maana kwamba hali ya mwanadamu ya kutengwa na Mungu inabadilishwa na sasa mwanadamu anaweza kuokoka (2 Wakorintho 5:19-21). Msingi wa upatanisho wetu ni mauti ya Kristo (Warumi. 5:10-11). Ni lazima tuweke sawa hapa kwamba ni mwanadamu tu ndiye anayebadilishwa. Mungu huwa habadiliki kamwe.

Hili jambo lina maana gani leo? Mungu sio adui yetu. Mungu huwa hakai pale akisubiri kwamba tutengeneze uadui tena. Yeye ni Rafiki yetu. Anatutaka tuuamini huo urafiki. Hawezi kutuachia sisi ambao tumeweka imani yetu katika Kristo Yesu.

Kipatanisho

Neno hili linatokea mara tatu katika matoleo kadhaa ya Biblia: Warumi 3:25; 1 Yohana 2:2, 4:10. Neno hili linajitokeza pia katika hali ya kutenda. Limetafsiriwa kwamba ni “kufanya upatanisho.”

Maana nzuri inaelezea kuwa ni mtu anayeondosha ghadhabu (ya Mungu).

Katika hali ya kitendo inapatikana katika Waebrania 2:17 na Luka 18:13.

Neno Hilasterion katika Kiyunani lilitumika katika nakala za kale za Maandiko kuelezea kiti cha rehema. Kifuniko cha Sanduku la Agano kilitengenezwa kwa dhahabu. Makerubi wawili waliangaliana na kuangalia chini wakikitazama kiti cha rehema. Shekinah, utukufu wa Mungu ulilikalia Sanduku. Kwenye Siku ya Upatanisho, Kuhani Mkuu alinyunyiza damu katika mfuniko kwa ajili ya dhambi za watu. Mungu alipoiona damu, aliachilia rehema badala ya hukumu. Haki yake ilipatikana. Kuleta kipatanisho ilimaanisha kumridhisha Mungu. Ni kwa nini Mungu anataka kusuluhishwa? Mungu amemkasirikia mwanadamu kwa sababu ya dhambi yake (Warumi 1:18, Waefeso 5:6). Damu ya Yesu iliyomwagika ilitupatanisha na Mungu (Warumi 3:25), na kuepusha ghadhabu yake na hili limetuwezesha kupokelewa katika familia yake, sisi ambao tumeweka imani yetu katika Yule aliyempendeza. Ukuta ambao dhambi iliujenga kati ya Mungu na mwanadamu umebomolewa. Upatanisho umefanywa kwa ulimwengu wote (I Yohana 2:2). Kusema kwamba Mungu amepatanishwa na sisi ina maana kuwa ameridhika.

Je, hili lina maana gani kwako na kwangu leo? Hatuhitaji kufikiri jinsi ya kulipia makosa yetu tuliyoyafanya. Nia yetu ya kufanya matendo mema, kutoa sadaka au kujitolea katika mambo mbalimbali sio kumpatanisha Mungu na sisi, lakini ni kwa sababu mioyo yetu imejawa na shukrani. Mungu ameridhika kabisa na upatanisho alioufaya Yesu Kristo.

Kuhesabiwa Haki—kuokolewa kutoka katika adhabu ya dhambi.
Kuhesabiwa Haki: tendo la mara moja tu.

Warumi 3:26, 5:1: Hili ni kama Tamko la ki-mahakama kwamba HAKUNA HATIA. Hakuna uwezekano wa kuhukumiwa huko mbeleni (Warumi 8:1). Hiyo ni nusu tu ya kwanza. Kisha Mungu anatupatia haki ya Kristo. Anatuhesabu kuwa tu wenye haki. Maisha makamilifu ya Kristo na kifo chake kwa ajili ya upatanisho ndio msingi wa kuhesabiwa haki kwa imani pekee. Tunapoamini, yote yaliyo ya Kristo, Mungu huyahesabia kwetu; nasi tunasimama tukiwa hatuna hatia. Hatuhesabiwi haki tu kwa kuwa tunaamini—hii ingefanya imani yetu iwe ndiyo imefanya kazi. Imani ni mkono mtupu ambao unampokea Mwokozi.

Kwa nini ni muhimu kwa sisi kuelewa kuwa ni watu waliohesabiwa haki? Hii haimaanishi kwamba hatuwezi kutenda dhambi tena. Huwa tunatenda dhambi. Na huwa tunakutana na madhara ya dhambi hapa hapa duniani kwa dhambi tulizozifanya. Lakini HAKUNA HUKUMU YA ADHABU MILELE. Jambo hili linapaswa litupe ujasiri katika mahusiano yetu na Mungu. Mungu hawezi kusema uongo. Kama akisema, “Huna hatia” na “Hakuna adhabu,” anasema ukweli na tunaweza kuishika ahadi Yake.

Namsikia Mshitaki akinguruma
Kwa mambo niliyoyafanya
Nayajua na mengine elfu nimefanya
Yehova hakuyaona!

Utakaso—kuokolewa kutoka nguvu ya dhambi
Utakaso: mchakato endelevu

1 Wathesalonike 4:3, 1 Petro 1:16

Kwenye Nafasi: Mwamini ametakaswa katika nafasi yake kwenye familia ya Mungu.

Kwa uzoefu: Kuendelea kutakaswa katika maisha ya kila siku (1 Petro 1:16)

Dhambi haitatutawala kama tutatambua kwamba tunaongozwa na Roho Mtakatifu. Ataendelea kutuweka huru kutoka katika matendo yetu ya nyuma. Atatupa nguvu ya kukataa vishawishi kwa kuwa tumemruhusu atuongoze. Je, unaziona safu zilizoko katika wokovu wetu? Mungu amekwishatengeneza mazingira ambayo yatatuwezesha kuishi maisha yanayompendeza yeye. Mungu tayari ameshatunza dharura yoyote inayoweza kutokea. Kwa hali hii tunaweza kuendelea kukua katika Kristo katika siku zote za maisha yetu.

Kutukuzwa—kuokolewa na uwepo wa dhambi
Kutukuzwa: tendo la mara moja

I Yohana 3:1-3; 1 Wakorintho. 15:35-56: Tutapokea miili yetu ya ufufuo, kama mwili wa Kristo. Hauna asili ya dhambi. Ni vigumu hata kuwaza jinsi miili hiyo ilivyo, tunaweza? Hii ni hali yetu ya baadaye. Ndio maana tunatakiwa kuyaangalia maisha yetu hapa duniani yenye mateso, maumivu, huzuni na majenzi kupitia dirisha ambalo tunauona Umilele. Miaka 30, 40, 50, 60, 70 au 80 hapa duniani ni kitu kidogo sana ukilinganisha na miaka ya milele. Miaka hii Mungu ametupa ili tuitumie kujiandaa kwa ajili ya maisha ya milele. Maamuzi tunayoyafanya hapa, chaguzi na vipaumbele vyote vinabeba sura ya maisha ya baadaye. Tunapaswa kuacha kuishi kana kwamba maisha ya hapa duniani ndio maisha pekee. Sisi tuliompokea Kristo ni watoto wa Mungu, kwa hiyo tunalindwa, Tunapendwa na tumehakikishiwa urithi wa mbinguni.

Kuzaliwa Upya: Kuzaliwa mara ya pili, kuzaliwa na Mungu, Kuzaliwa kwa Roho

Yohana 3:3, 7; 1 Petro 1:3, 23; Yohana 1:13; Tito 3:5: Mara tu tunapomwamini Kristo tunapewa uzima (maisha mapya) wa milele: ambao ni maisha ya Mungu katika moyo wa binadamu. Uzima huu ni wa mara moja na haufutwi wala kurudiwa. Ni kuwa hai kutoka wafu na kupata kwa ubora kabisa maisha na kusudi jipya la kuishi (2 Wakorintho 5:15, 17).

Msamaha wa dhambi

Waefeso 1:7, Yohana 1:29: Msamaha ina maana ya kuondolewa, kama ilivyokuwa kwa kondoo wa kafara kwenye Mambo ya Walawi 16.

Msamaha wa Mungu sio sawa na misamaha yetu. Mungu alijua kwamba sisi hatuwezi kujisikia kukubalika naye au kuwa huru kumtumikia ikiwa ndani yetu tumebeba hatia na hukumu kwa sababu ya dhambi zetu za zamani katika dhamiri zetu. Alijua kwamba dhambi zetu zinapaswa kuondolewa kabisa. Hilo ndilo Yesu alilolifanya kwa kuichukua adhabu yetu. Hii ni kweli na sio kwa ajili ya dhambi tulizozifanya kabla ya kumpokea Kristo, bali kwa ajili ya dhambi tutakazofanya leo na kesho.

Msingi wa Kutakaswa kwa Mwamini

Damu ya Kristo iliyomwagika mara moja tu ndio msingi wa kutakaswa kwetu mara kwa mara kutoka dhambi (1 Yohana 1:7-9). Uhusiano wetu wa kifamilia unashikiliwa na kifo chake; ushirika wetu hurejeshwa kwa kuungama kwetu.

Je, hili lina maana gani kwetu? Hii ina maana kwamba mambo ya kale yalishasamehewa na tunaweza kuendelea kutembea na Mungu kuanzia sasa. Kuungama hapa ina maana ya kukubaliana na Mungu, ya kwamba akisema hii ni dhambi na sisi tunasema hii ni dhambi. Usianze kuitetea: Ooh nilikasirishwa, nilimjibu hivyo kutokana na tabia yake chafu; nina mume asiyejituma n.k Wewe sema, Nilidanganya, Niliiba, Nilimsema vibaya, Nilimjeruhi, Nilikosa upendo. Kiri au ungama jambo kama lilivyo. Kisha Mungu husamehe kwa sababu Yeye ni mwaminifu na wa haki. Mwaminifu maana yake ni kwamba, kwa kuwa alisema, basi atafanya. Wa Haki maana yake ni kwamba kwa kuwa adhabu ililipwa na Mwanaye, atakuwa sio wa haki kutudai tulipe tena. Hili ndilo jambo linalotokea Mungu anapotusamehe dhambi zetu.

Atazitua nyuma yako—Isaya 38:17
Hatazikumbuka—Yeremia 31:34
Ataziweka Mbali nawe—Zaburi 103:12, Mika 7:19
Hizo dhambi hazipo—Isaya 43:25-44:22
Dhamiri imetakaswa—Waebrania 9:14, 10:22

Je, wewe na mimi tunawezaje kuyaona haya? Tunapoziungama dhambi zetu, tunapaswa kuamini kwamba Mungu amesamehe na kututakasa, kisha kwa kuamua tu, tunaupokea msamaha Wake.

Nimemwona Mungu akiwafungua watu kutokana na hatia na aibu ya dhambi zilizopita kwa tendo hili rahisi tu. Hili linaonyeshwa kupitia mwanamke aliyefanya uzinzi mara moja.

Asili ya dhambi imehukumiwa

Warumi 6:1-10, 14: Kifo hakina maana ya kwisha au kumalizika, lakini ni kutenganishwa. Kusulubiwa kwa Mkristo pamoja na Kristo ina maana ya kutengwa na utawala wa dhambi katika maisha yake. Asili ya dhambi haifanyi tena kazi katika maisha yake. Kusulubiwa pamoja na Kristo pia ina maana ya kufufuka pamoja naye kuyaingia maisha mapya. Warumi 6:4: Matendo ya kihistoria ya Kifo cha Kristo na kufufuka vinakuwa sehemu ya historia yetu wakati tunapookoka. Utawala wa asili yetu ya dhambi unaangushwa na kifo cha Kristo nasi tunakuwa huru kuishi maisha yanayompendeza Mungu.

Jambo hili lina maana gani kwetu leo? Mkanda unaotuunganisha sisi na asili ya dhambi unakuwa umekatwa. Sasa tunaweza kukaa chini ya utawala wa Roho Mtakatifu na kumruhusu atengeneze tabia mpya ndani yetu. Nguvu ya dhambi za zamani kama tamaa, wivu, uzinzi, uchoyo, hasira, matusi na mengine—yanaweza kuvunjwa na tukatambua kwamba tumefufuliwa pamoja na Kristo ili tuishi maisha ya ushuhuda mzuri. Tumekuwa viumbe vipya (2 Wakorintho 5:17).

Msingi wa kuondolewa dhambi za Kabla ya Msalaba

Je, ni nini ulikuwa msingi wa msamaha kwa watakatifu wa Agano la Kale? Damu ya wanyama hufunika tu dhambi. Lakini Mwana Kondoo wa Mungu anaondoa dhambi ya ulimwengu. Hakuna kushughulikia dhambi kulikofanikiwa kabla ya msalabani. Kifo cha Kristo ndio msingi wa msamaha katika kila kizazi; imani ni njia tu ya kuufikia. Kitu ambacho hatukijui ni kiasi cha imani kilichokuwa kinahitajika katika Agano la Kale. Lakini kwa kuwa Kristo ni Mwana Kondoo aliyechinjwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu (1 Petro 1:20), katika macho ya Mungu ilikuwa tayari imekwishafanyika, kwa kuwa Mungu haathiriwi wala kufungwa na muda. Hata kama watakatifu wa Agano la Kale hawakuwa na ufunuo mkamilifu ambao sisi tunao sasa, walichukua hatua ya imani kufanya kile ambacho Mungu aliwaagiza kufanya. Walileta dhabihu walizoagizwa na walisamehewa kwa sababu Mungu alijua kwamba angewatolea Mwana Kondoo mkamilifu siku moja.

Kukaliwa na Roho Mtakatifu

Yeye hukaa ndani yetu muda wote ili kutuumbia tabia ya Kristo ndani yetu. Hutupa nguvu za kushinda majaribu. Hulitia nuru Neno la Mungu, hutuongoza katika mapenzi ya Mungu. Tunakaliwa na Mungu Mwenyewe (Waefeso 4:6, Wagalatia 2:20, 1 Wakorintho 6:19, Warumi 8:9).

Kuasilishwa (Adoption)

Wagalatia 4:1-5, Warumi 8:14-17: Kuasilisha mtoto. Katika utamaduni huo, mtoto, kwamba amezaliwa katika familia au la, alipewa haki zote na majukumu ambayo yanamkabili katika familia husika.

Sisi ni watoto tuliozaliwa katika familia ya Mungu na kwa kuwasilishwa sisi ni wana na mabinti tulio na haki zote. Kuasilishwa huku kunatupa hadhi mpya.

Matokeo ya kuwasilishwa ni kukombolewa kutoka utumwani, kutoka dhambi na mwili.

Urithi

Hii ni pamoja na kukamilika katika Kristo (Wakolosai 2:9-10), tukiwa na kila baraka ya kiroho (Waefeso 1:3), na uhakika wa kwenda mbinguni (1 Petro 1:3-5)

Mwisho wa Torati

Warumi 10:4, Wakolosai 2:14: Torati humwonyesha mwanadamu hitaji lake la kumhitaji Kristo (Wagalatia 3:21-24), lakini haiwezi kuhesabiwa haki au kukufanya uwe safi. Sisi tunaishi chini ya sheria ya Kristo (Wagalatia 6:20), au sheria ya Roho (Warumi 8:2). Amri zote Kumi zimerudiwa katika Agano Jipya isipokuwa ile ya Sabato.

Je, hili lina maana gani kwetu? Amri Kumi ziliandikwa katika vibao vya mawe. Sheria ya Kristo Imeandikwa katika mioyo yetu na tunakuwa makini kuhakikisha kwamba tunajifunza Neno na kutii miguso ya Roho Wake.

Torati au Sheria inasihi,
Fanya Hivi ukaishi,
Mikono na Miguu hupewi,
Neno jema yaleta Injili,
Hutugusa turuke angani

Kuna watu ambao wanataka kuturudisha tukae chini ya Torati. Mambo mengine wanayotuambia yanaweza kuwa hayana madhara. Lakini mara tu mtu anapoleta sheria ili apime kiwango cha hali yetu ya kiroho, kama vile kutokula nguruwe au kutokunywa kahawa ni lazima tuwe macho. Baadhi ya mawazo haya hutokana na imani potofu, lakini mengine hutokana na Wakristo wanaotaka kupima kuwa mtu wa kiroho yukoje. Usimruhusu mtu yeyote akuweke chini ya Torati. Kristo aliitimiliza Torati kwa kuitii kikamilifu na kisha akachukua adhabu ya wote walioshindwa kuitii.

Msingi wa hukumu ya Shetani

Wakolosai 2:15, Yohana 12:31, Waebrania 2:14: Hukumu zote anazohukumiwa Shetani msingi wake ni ushindi ambao Kristo aliupata msalabani. Shetani ni adui aliyeshindwa.

Hili lina maana gani kwetu? Kabla ya wokovu, tulimilikiwa na ufalme wa Shetani. Tulipompokea Kristo, Mungu alituhamisha na kutuingiza katika Ufalme wa Mwanawe Mpendwa (Wakolosai 1:13). Alikuja akakaa ndani yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Aliyeko ndani yetu ni mkuu kuliko Huyo aliyeko katika dunia. Usimfikirie sana Shetani. Wewe elewa tu kwamba una adui ambaye ameshindwa ambaye anajaribu kukushika kisigino ili nawe uwe ni Mkristo aliyeshindwa ambaye hana nguvu ya kumshuhudia Kristo. Tambua hila zake bila kunaswa nazo. Wewe sio mali yake tena.

Kwa kiwango gani?

Thamani au kiwango cha kifo cha Kristo ni kubwa sana na haipimiki. Kilikuwa ni kwa ajili ya watu wote na ni kwa muda wote. Lakini kina maana na thamani tu kwa wale wanaomwamini (Yohana 1:29, 3:17; 2 Wakorintho 5:19; 1 Timotheo. 4:10; 2 Petro. 2:1; 1 Yohana 2:2).

Wokovu unapatikanaje?

Kama mara elfu mbili katika Agano Jipya, wokovu unapatikana katika msingi wa imani katika Bwana Yesu Kristo ambaye alikufa kwa ajili ya dhambi zetu (Yohana. 3:16, 1:12; Matendo 16:31). Wokovu ni karama ya bure. Na inapaswa ipokelewe. Hakikisha kuwa mtu anaelewa kabla ya kumfanyia maombi.

Jadili hatari ya kumshinikiza mtu kwa kumwalika kumpokea Kristo.

Ulinzi wa Nje

Ushahidi:

  1. Roho Mtakatifu hutuweka katika Mwili wa Kristo—kwa ubatizo (1 Wakorintho 12:13). Hakuna mawazo kwamba tunaweza kuondolewa.
  2. Roho Mtakatifu humtia muhuri mwamini hadi siku ya ukombozi (Waefeso 1:13; 4:30). Hii ni alama ya umiliki na mamlaka. Kupoteza wokovu kungekuwa na maana ya kuuvunja muhuri kabla ya siku ya ukombozi.
  3. Roho Mtakatifu ni malipo ya awali au arabuni ambayo tunaipokea katika wokovu wetu (2 Wakorintho 5:5, Waefeso 1:14).
  4. Ni ahadi ya Yesu (Yohana 10:28-30).
  5. Warumi 8:28-39 ndiyo inayoshawishi zaidi na ina maelezo.

Maswali ya Kujifunza

Soma Waefeso 1:3-14; Warumi 8:28-30

1. Wokovu wetu ulipangwa lini? Ni nini kusudi la Mungu kwetu sisi tuliompokea Kristo? Ni nini matokeo yake (6, 12, 14)?

Soma Waebrania 9:22, 26-28; 10:11-14

2. Kwa nini sadaka za kuteketezwa zilitolewa? Kwa nini sadaka za wanyama hazikutosha? Kwa nini sadaka ya Kristo ilikuwa ni muhimu?

Soma Mathayo 20:28: Marko 10:45; 1 Petro 3:18

3. Ni nini maana kuu ya Kifo cha Kristo? Andika kwa kifupi kwa kutumia maneno yako mwenyewe kwamba kinamaanisha nini kwako binafsi.

Soma 1 Wakorintho 15:1-4, 12-19

4. Kwa ufupi injili ina maana gani? Kwa nini kufufuka kwa Yesu kulikuwa ni kwa muhimu?

Waefeso 1:19-23; Waebrania 7:23-27

5. Yesu yuko wapi sasa? Ni nini huduma yake ya kimbingu kwetu leo?

Soma 1 Wakorintho 6:20; 1 Petro 1:18-19; Wagalatia 3:13; Tito 2:14

6. Je Kristo alitimiliza nini kwa ajili yetu katika mistari hii? Ni nini kusudi lake kwa ajili ya maisha yetu?

Soma 2 Wakorintho 5:17-21

7. Ni kitu gani kingine kilichotimilizwa kwa ajili yetu?

Soma Wakolosai 1:13-14; I Yohana 1:7; Waebrania 9:14

8. Ni kitu gani kingine kilichotimilizwa kwa ajili yetu? Ni kwa jinsi gani tunaweza kusamehewa dhambi tulizozifanya baada ya kuokoka? Je Mungu anatutaka tuendelee kubeba hatia ya dhambi iliyokwishasamehewa? Kwa nini?

Soma Wafilipi 3:20; 1 Petro 2:5, 9; Yohana 1:12-13; Wagalatia 4:5; 1 Petro 1:4

9. Orodhesha faida nyingine za wokovu wetu ambazo zinapatikana katika aya hizi

Soma Warumi 8:31-39

10. Ni kitu gani ambacho ukikifanya utapoteza uhusiano wako na Mungu? Je, kuna jambo lolote ambalo mtu mwingine anaweza kufanya kwako ili kufuta kila kitu ambacho Kristo amefanya? Una maelezo gani kwa swali hili? Je, hali hii inakufanya ufikiri kuwa ni sawa tu kutenda dhambi kwa vile kuna kusamehewa? Au je, inakuhimiza kumpenda Bwana zaidi na kumtumikia kwa uaminifu zaidi?

Related Topics: Curriculum, Hamartiology (Sin), Soteriology (Salvation)

Report Inappropriate Ad