MENU

Where the world comes to study the Bible

Report Inappropriate Ad

Meza ya Bwana na Krismasi

Related Media

Nilipokuwa nasoma chuoni, nilikuwa na kazi mbili ambazo nilikuwa nazifanya ili kujipatia kipato. Moja ilikuwa ni kufanya kazi katika karakana ya magari, na nyingine ilikuwa ni kuuza barafu kutoka kampuni ya Maziwa, mkabala tu na pale kwenye kazi ya kwanza. Kwa kweli niliuza barafu zilizoganda za maziwa, zenye vijiti na zilizo na chokoleti. Niliendesha kigari kilichofungiwa jokofu kwa nyuma. Nilikuwa nimekaa mbele na milango miwili imefunguliwa, watoto walinifuata kwa hamu na wakati mwingine mbwa wa jirani ambao hawakuwa rafiki sana.

Tatizo lililojitokeza ni kwamba ratiba yangu kule kwenye karakana iligongana na ile kule kwenye kampuni ya maziwa. Kwa kuwa baba yangu hakuwa na ufundi katika magari, alinisaidia kwenda kuuza barafu. Sasa uelewe kwamba baba yangu alikuwa ni Mkurugenzi wa shule ya msingi na pia ni mwalimu. Kwa kweli huu ni unyenyekevu wa pekee kuendesha kile kigari cha barafu na kuzunguka nacho huko mjini, akiwauzia watoto barafu huku akiwafukuza mbwa waliokuwa wakimfuata.

Siku moja naona baba alinyenyekea sana. Mwanamke mmoja alikuja kununua barafu na alipokaribia kile kigari, alimtambua baba yangu. Alishangaa sana na baba naye alimtambua vizuri – alikuwa ni mke wa mjumbe wa bodi ya ile shule. Kwa bahati, baba alimwelewa na haraka alimwambia, “Hivi unaweza ukamsaidia mtoto akiwa chuoni?”

Unaweza ukashangaa kwamba simulizi hii inahusianaje na meza ya Bwana, au kurudi kwa Bwana wetu, ambako huwa tunakusherehekea wakati wa Krismasi. Nadhani nitakuelezea jinsi yanavyohusiana katika mafundisho haya.

Kuna baadhi ya watu wanaoamini kwamba vifaa – yaani mkate na mvinyo (au divai) – tunavyovitumia wakati wa meza ya Bwana, ni zaidi ya vitu tu. Wanaamini kwamba kwa njia fulani ya kimiujiza kwamba mkate na mvinyo hubadilika na kuwa mwili na damu ya Bwana wetu. Najaribu kuwaza kwamba kama sivyo, hivi ni vitu tu vya kawaida vya kutumia. Kwa upande mwingine tunaamini kuwa mkate na mvinyo ni alama tu. Naomba niseme tu kwamba hizi alama ni za muhimu sana na zina maana kubwa, kama tu tukizielewa.

Kimsingi nitajikita kwenye mkate, ambao tunautumia kwenye meza ya Bwana, kwa sababu ninaamini kwamba unawakilisha Bwana wetu kufanyika mwili. Ningependa kukufahamisha namna mbili ambazo ule mkate wa meza ya Bwana ni alama ya kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwanza, ni alama ya kwamba Bwana wetu alizaliwa bila dhambi. Hakuna mtu mwingine katika historia mwenye hiyo sifa, hakuna, hata mtu mkubwa kama mfalme Daudi. Ni Daudi ndiye aliyeandika,

Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani (Zaburi 51:5).1

Na bado Bwana wetu angeweza kusema.

“Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli mbona ninyi hamnisadiki?” (Yohana 8:46, msisitizo ni wa kwangu)

Kuna sababu ya muhimu sana  kwamba kwa nini Bwana awe hana dhambi. Mtakumbuka kwamba katika Agano la Kale Wayahudi waliagizwa watoe dhabihu za wanyama wale tu ambao walikuwa “hawana ila wala waa”.

17Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 18Nena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote, uwaambie, ‘Mtu yeyote wa nyumba ya Israeli, au wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni nadhiri zao mmojawapo, au kama ni sadaka yoyote ya hiari, watakayomtolea Bwana kuwa sadaka ya kuteketezwa; 19ili mpate kukubaliwa, mtaleta mume mkamilifu, katika ng’ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi. 20Lakini mnyama yeyote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu. 21Na mtu awaye yote atakayemtolea Bwana dhabihu katika zaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng’ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema ndani yake chochote. 22Kipofu au aliyevunjika mahali, au kiwete, au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na kikoko, hamtamtolea Bwana wanyama hao, wala msiwasongeze kwa Bwana kwa njia ya moto juu ya madhabahu.” (Walawi 22:17-22, msisitizo ni wa kwangu)2

Mwana kondoo wa Pasaka alipaswa kuwa hana ila (Kutoka 12:5), na hii ilikuwa ni taswira halisi ya Masihi (Yesu) ambaye alikuwa anakuja baadaye.

18Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; 19bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani ya Kristo. (1 Petro 1:18-19, msisitizo ni wangu)  

Yesu hakuzaliwa akiwa na asili ya dhambi, kama jinsi tulivyokuwa sisi. Alizaliwa akiwa hana dhambi ya aina yoyote. Shetani alijaribu kwa kila njia kumtia Bwana wetu majaribuni ili atende dhambi, lakini alishindwa, na Bwana wetu alimshinda (Mathayo 4:1-11; Luka 4:1-12). Yesu hakuwa na dhambi na ndio maana aliweza kuchukua dhambi yetu mwilini mwake, akabeba adhabu iliyotustahili sisi, na akawa ni wokovu kwa wote watakaomwamini:

4Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejivika huzuni zetu
Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu, na kuteswa,
5Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6Sisi sote kama kondoo tumepotea;
Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe;
Na Bwana ameweka juu yake maovu yetu sisi sote.
7Alionewa lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake;
Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo
Mbele yao wakatao manyoya yake; naam hakufunua kinywa chake.
8Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa;
Na maisha yake ni nani atakayesimulia?
Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;
Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;
Na pamoja na matajiri katika kufa kwake;
Ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na ila kinywa kinywani mwake.
10Lakini Bwana aliridhika kumchubua; amemhuzunisha;
Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,
Ataona uzao wake ataishi siku nyingi,
Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;
11Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika.
Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki,
Atawafanya wengi kuwa wenye haki; naye atayachukua maovu yao.
12Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu,
Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari;
Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa,
Akahesabiwa pamoja na wakosao.
Walakini Alichukua dhambi za watu wengi,
Na kuwaombea wakosaji.” (Isaya 53:4-12)

Mtume Paulo analiweka hivi:

17Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita – tazama, yote yamekuwa mapya! 18Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; 19yaani Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ameweka ndani yetu huduma ya upatanisho. 20Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kama kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. 21Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (2 Wakorintho 5:17-21, msisitizo ni wangu).

Mwandishi wa kitabu cha Waebrania aliandika:

11Lakini Kristo akiisha kuja, aliye Kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu,  12wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kufanya ukombozi wa milele. 13Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa na kuusafisha mwili; 14basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai? (Waebrania 9:11-14, msisitizo ni wangu)

Yakobo anatukumbusha kwamba Mungu hawezi kujaribiwa na dhambi. Kwa kuwa Bwana wetu Yesu ni Mungu, hawezi kujaribiwa na dhambi:

Mtu ajaribiwapo asiseme, “Ninajaribiwa ma Mungu,” maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu (Yakobo 1:13, msisitizo ni wa kwangu).

Mtume Petro anasisitiza kuwa Bwana wetu Yesu Kristo hana dhambi, hali iliyomfanya aweze kutufia, akachukua adhabu ya dhambi zetu:

21 Kwa sababu ndio mlioitiwa, maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. 22 Yeye hakutenda dhambi wala hila haikuonekana kinywani mwake. 23 Yeye alipotukana hakurudisha matukano; alipoteswa hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. 25 Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu (1 Petro 2:21-25).

Tunaposhiriki Meza ya Bwana, mkate tunaoutumia ni mkate usiotiwa chachu. Hauna hamira kabisa maana hamira ni alama ya dhambi. Katika hili Mtume Paulo aliandika:

6Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachua donge zima? 7Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; 8basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli (1 Wakorintho 5:6-8).

Baada ya kusherehekea Pasaka (wakati kondoo wa Pasaka alipochinjwa na kuliwa), Karamu ya Mikate isiyochachwa ilianza na ilidumu kwa wiki moja. Familia za kiyahudi hutafuta katika nyumba yote ili kuona kama kuna hamira au chachu yoyote na kisha kuitoa nje. Dhabihu ya mwana-kondoo wa Pasaka ilikusudiwa kuondoa chachu. Paulo anatumia alama hii anapoelezea uchafu katika maisha ambao ulikuwa ukifanywa—katika kanisa la Korintho. Paulo anawakumbusha wao na sisi kwamba Yesu alikuwa ni Mwana-kondoo wa Pasaka, na kwa kuwa alikwishatolewa, tusiendelee kukumbatia dhambi. Kristo hakuwa na dhambi, na alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa hiyo inatupasa kuondokana na dhambi kwa sababu ya Yesu.

Kutokana na hili tunapaswa kumtambua Masihi (Yesu) anatakiwa awe hana dhambi, ili aweze kufa kwa ajili ya wengine, na sio kufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe. Kwa njia, hii Mungu anaweza kutusamehe dhambi zetu kwa msingi wa kile Yesu alichofanya kwa ajili yetu. Lakini ni kwa vipi Yesu anaweza kuja ulimwenguni huku bila dhambi, ilhali kila mtu aliyezaliwa alizaliwa na dhambi? Hii ndio maana alizaliwa na bikira. Kusherehekea kwetu Krismasi kunatukumbusha jinsi Yesu alivyoweza kuja humu duniani akiwa Mungu na pia akiwa ni mwanadamu lakini akiwa hana dhambi. Mariamu alikuwa ni mama yake Yesu lakini Yusufu alikuwa sio baba yake. Roho Mtakatifu ndiye aliyemfanya Mariamu kuwa mjamzito. Kuzaliwa na bikira kulimaanisha kuwa Yesu alizaliwa akiwa hana dhambi. Hii ilimaanisha kuwa ni Yeye tu, na ni Yeye pekee ambaye angeweza kuwa Masihi. Aliweza kufa kwa ajili ya dhambi zetu kwa sababu hakuwa na dhambi za kwake.

Tunapoushiriki mkate katika Meza ya Bwana, tunapaswa kukumbuka uzao wa bikira aliozaliwa nao Bwana wetu na kwamba Yesu hakuwa na dhambi. Yeye alikuwa ni “Mwana-kondoo wa Mungu asiye na waa,” na kwa sababu hii, aliweza kufa msalabani, akaimwaga damu yake ya thamani kwa ajili ya dhambi zetu. Bila hali ya kutokuwa na dhambi ya Yesu, ambayo alama yake ni mkate, kifo chake kungekuwa hakina thamani kwetu. Kwa hiyo habari ya Krismas ni muhimu kwa ajili ya wokovu wetu, na kwa Meza ya Bwana, ambayo inasherehekea wokovu ambao Mungu aliutoa kwa ajili yetu ndani ya Yesu.

Mkate ni alama ya kitu kingine, ninavyoamini. Ni alama ya unyenyekevu wa Yesu kuja duniani kama mwanadamu. Sehemu nyingi duniani, mkate ni chakula cha msingi sana. Waisraeli walipokuwa jangwani kwa miaka arobaini, Mungu aliwalisha kwa mana (mkate) na maji. Ndio maana Waisraeli walilalamika kwamba Mungu aliwapa mana ambayo ilikosa ladha na wakatamani kama wangepata kitu kingine ambacho kilikuwa na kadha nzuri zaidi:

4 Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena wakasema, “Ni nani atakayetupa nyama tule? 5 Tunakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitumguu, na vitunguu saumu; 6lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu chochote; hakuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu! (Hesabu 11:4-6)

Kulipokuwa na njaa kali katika nchi ya Israeli, Mungu alimtuma Eliya kuishi na mjane wa watu wa mataifa akiwa na mwanaye. Eliya aliwaendea wakiwa wanajiandaa kula mlo wao wa mwisho—ambao ni mkate mdogo na maji:

8 Neno la Bwana likanijia kusema, 9 “Ondoka uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.” 10 Basi akaondoka, akienda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita akamwambia, “Niletee nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.” 11Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, “Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako,” 12 Naye akasema, “Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chombo. Nami ninaokota kuni mbili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu; tuule tukafe.” 13 Eliya akamwambia, “Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli asema hivi, ‘Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.’” 15 Basi akienda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. 16Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya (1 Wafalme 17:8-16).

Hakuna chakula kilichokuwa rahisi na ambacho kinaweza kuitwa mlo kuliko mkate na maji. Kumbuka kwamba huu ulikuwa ni mkate usiochachwa. Hatuongelei maandazi au kalimati; tunaongelea kitu kama chapati za kusukuma. Ni kwa nini Mungu alichagua mkate – ambacho ni mlo rahisi kuwakilisha kuja kwa Mungu katika mwili wa kibinadamu, katika kutuokoa kutoka katika dhambi zetu? Naamini kwamba mkate ni alama ya unyenyekevu wa Bwana wetu. Isaya aliposema juu ya Masihi anayekuja, alimzungumzia Mtu ambaye hataangaliwa kama binadamu asiye wa kawaida, bali kama Mtu ambaye angepuuzwa kama ambaye sio wa muhimu:

1 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? 2 Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo, na kama mzizi katika nchi kavu; yeye hana umbo wala uzuri; na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani,  3Alidharauliwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu (Isaya 53:1-3 msisitizo ni wangu).

Mika, aliyehudumu wakati wa Isaya, alisema juu ya mahali pa kuzaliwa Masihi kama sio muhimu:

2 Bali wewe Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele. 3 Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli. 4 Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia (Mika 5:2-4, mkazo ni wangu).

Yesu alizaliwa katika mji usio maarufu kama Bethlehemu, na sio Yerusalemu. Alipokuwa akikua, Yesu aliishi Nazareth, mji ambao hawatokei watu maarufu:

19 Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, 20 akasema, “Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.” 21 Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. 22 Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, 23 akaenda akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo. (Mathayo 2:19-23, msisitizo ni wangu)

Yesu alipoanza huduma yake hadharani, Filipo alimwona Nathanaeli na kumwambia kuwa wamemwona Masihi. Tatizo lilikuwa kwamba Yesu alikuwa Mnazorayo, na Nathanaeli haikuweza kuamini kwamba Masihi anaweza kutokea sehemu ya kawaida kama hiyo:

44 (Naye Filipo alitokea Bethsaida, ambao ni mji wa Andrea na Petro.) 45 Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, “Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, -- Yesu mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareth.” 46 Nathanaeli akamwambia, “Laweza neno jema kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone” (Yohana 1:44-46, mkazo ni wangu).

Katika maandiko hapa chini kwa Wafilipi, Mtume Paulo anakaza juu ya unyenyekevu wa Bwana wetu kuja duniani:

4 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. 5 Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; 6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; 7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; 8 tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya msalaba! (Wafilipi 2:4-8)

Katika maombi yake kama Kuhani mkuu kwenye Yohana 17, Mwana wetu alizungumzia utukufu aliokuwa nao na Baba kule mbinguni kabla ya kuja duniani (hata kabla dunia haijakuwepo).

4Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza ile kazi uliyonipa nifanye. 5 Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. 6 Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. (Yohana 17:4-6 mkazo ni wangu)

Hebu fikiria, Mwana wa Mungu anauacha utukufu wa mbinguni na anakuja kuishi katika hii dunia iliyojazwa na dhambi, anadharauliwa na watu, na hatimaye anasulubiwa kama mhalifu! Krismasi inahusu Mungu Mwana kujinyenyekeza na kuja duniani kama mwanadamu. Alikuja, sio kama tajiri mwenye nguvu, bali kama mtoto katika hali ya umaskini. Unyenyekevu wa mwisho ulikuwa ni mateso na aibu katika mikono ya watu wenye dhambi walipomsulubisha kama mhalifu, mhalifu mbaya kuliko Baraba, mwizi, mchochezi na mwuaji.

Nilianza ujumbe huu kwa kisa cha baba yangu aliyejinyenyekeza hadi kufikia kuendesha kigari cha kuuzia barafu. Alilofanya hili kwa ajili yangu, kwa kuwa mimi ni mtoto wake. Yesu naye alijinyenyekeza kiasi cha kuiacha mbingu na kuja duniani kama mwanadamu – mwanadamu asiye na faida – akafa msalabani Kalvari kama mhalifu, badala yangu. Alilofanya hili kwa ajili yangu mimi na wewe ili tuweze kufanyika watoto Wake. Kwa wakati ule tulikuwa ni maadui zake, lakini akajinyenyekeza, akabeba dhambi zetu, na kufa badala yetu, ili tuweze kupokea msamaha wa dhambi na karama ya uzima wa milele.

Hatuwezi kushiriki meza ya Bwana bila kusherehekea habari ya Krismasi. Kwa hiyo hatusherehekei Krismasi mara moja kwa mwaka, ila ni kila wakati tunaposhiriki Meza ya Bwana.

Tunaposhiriki meza ya Bwana, vifaa vinapitishwa ambavyo ni mkate na kikombe mbele yetu. Ni lazima tuamue kuchukua mkate na kunywe mvinyo. Hizi ni alama tu kwa hiyo inatupasa kuamua kuwa tunaipokea kazi ya Yesu Kristo pale msalabani kwa niaba yetu. Je, tunamwamini Yeye kama mwana wa Mungu aliyekuja duniani katika mwili wa mwanadamu? Je, tunaamini kwamba alizaliwa na bikira kwa kazi ya Roho Mtakatifu, na kwa hiyo hakuchanganyikana na dhambi? Je, tunaamini kwamba, damu aliyoimwaga ilitokana na Mwana wa Mungu asiye na waa wala ila? Je, unakubali kwamba sisi ni wenye dhambi, ambao tumaini letu pekee ni kazi ya Yesu kwenye msalaba wa Kalvari? Ni lazima tumpokee Yeye kabla hatujazipata faida za kile alichokifanya. Natumaini kwamba utakuwa umelifanya hili. Kama bado hujafanya, nakuombea kwamba utalifanya leo na ukigundua furaha ambayo Krismas ilikusudiwa kuileta.

18 Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwachia kwa siri. 20 Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, “Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 21 Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” 22Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, 23 “Tazama bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana, nao watamwita jina lake Imanueli;” yaani, “Mungu pamoja nasi.” (Mathayo 1:18-23, msisitizo ni wa kwangu)

© 2020, Biblical Studies Foundation. All Rights Reserved. For copyright and usage details see: https://bible.org/permissions.


1 Nukuu za Maandiko zimetoka Biblia Takatifu (Union Version, 1952)

2 Kwa kulinganisha, Soma Malaki 1:6-8 ambapo watu wa Mungu wanaadhibiwa kwa kuleta wanyama wasiofaa kwa ajili ya sadaka

Related Topics: Communion

Report Inappropriate Ad