MENU

Where the world comes to study the Bible

Somo la 7: Kanisa

Related Media

Kanisa ni nini? Lilianza lini? Ni kwa nini kuna madhehebu mengi? Kundi hili linaabuduje katika kanisa la Biblia?

Neno kanisa kwa Kiyunani ni ekklesia. Neno hili lina maana ya, “kilichotengwa kwa kusudi maalum; kusanyiko.”

Jambo la kwanza la kujifunza ni kwamba Biblia inalizungumzia kanisa kwa namna mbili tofauti: Kanisa la ulimwengu wote kama mwili mmoja, na kanisa la mahali fulani kama taasisi.

Kanisa La Ulimwengu Wote – Mwili

Maana: Kanisa la Ulimwengu Wote ni jumla ya waamini wote wanaounda mwili wa Kristo kwa njia ya ubatizo kwa Roho Mtakatifu, na liliundwa siku ya kwanza ya Pentekoste, ni tofauti kabisa na taifa la Israeli na haliishii mahali fulani au dhehebu fulani tu.

Kila mtu, akiwa hai au amekufa, ambaye aliwahi kumpokea Yesu Kristo na kumwamini kama Bwana na Mwokozi wake, tangu siku ile ya Pentekoste hadi sasa, ni mmoja wa Kanisa la Ulimwengu, yaani mwili wa Kristo ambapo yeye, Kristo ndiye kichwa (Waefeso 1:22)

Yesu Alisema Nini Kuhusu Kanisa?

Soma Mathayo 16:18-19

Kristo alilizungumzia kama la wakati ujao

Kristo alipozungumza maneno haya, kanisa lilikuwa ni kitu cha wakati ujao kwa hiyo halikuwepo wakati akiwa hapa duniani. Je, ni nani msingi ambako kanisa limejengwa? Ni nani au ni nini ambacho ni mwamba, Kristo alichokuwa anaelezea?

Petro mwenyewe anasema kwamba Kristo ndiye Mwamba (1 Petro 2:4-8; 1 Wakorintho 3:11, hakuna msingi mwingine; Waefeso 2:20).

Au inaweza ikawa kwamba ukiri wa Petro, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai”, ndio mwamba, kwa sababu kila mtu anayejiunga na kanisa la ulimwenguni lazima aamini kwamba huu ndio ukweli kuhusu Yesu.

Kanisa Lilizaliwa Lini?

Soma: Matendo 1:5 na 2:1-4

Kanisa lilizaliwa siku ya Pentekoste, kama siku kumi hivi baada ya Yesu kupaa kwenda mbinguni. Roho Mtakatifu alishuka ili kumwingiza kila mwamini katika mwili wa Kristo na kumkalia kila mwamini kibinafsi kabisa. Pentekoste kwa Roho Mtakatifu ilikuwa ni kama Krismasi kwa Yesu. Alikuja kuhusianisha waamini wote kwa namna mbalimbali.

Paulo analizungumzia kanisa kama siri:

Soma Waefeso 3:6

Siri hii ni kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wanaungana na kuunda kitu kimoja kwa njia ya ubatizo wa Roho Mtakatifu. Sifa pekee kwa ajili ya kujiunga ni imani katika yule Mwokozi aliyefufuka. Kanisa ni kitu kipya kabisa ambacho huundwa na Wayahudi na Watu wa Mataifa.

Kwa hiyo ni wazi pia kwamba, kila mwamini tangu siku ya Pentekoste, akiwa hai au amekufa, ni kiungo katika mwili wa Kristo, ambao ni kanisa la ulimwengu wote. Waamini waliokwishafariki dunia wako pamoja na Bwana wakisubiri siku ambayo tutakuwa pamoja.

Kanisa La Mahali – Asasi

Maana. Kanisa la mahali ni kusanyiko la waamini waliojipambanua wanaofuata mapokeo fulani na mfumo fulani wa uongozi, na ambao wanaigusa jamii kwa ajili ya Kristo kwa njia ya kumwabudu Mungu hadharani, wakiwajenga waamini, na kuhubiri injili kwa waliopotea.

Kuna tofauti kati ya kanisa la ulimwengu wote na kanisa la mahali. Kanisa la ulimwengu wote lina waamini tu, lakini kanisa la mahali lina watu ambao wanadai kuwa ni waamini wakati kwa kweli hawaamini kabisa. Inawezekana ukawa muumini wa kanisa la mahali lakini ukawa sio mwamini katika mwili wa Kristo. Hii inafanyika kwa njia ya ujinga au udanganyifu. Baadhi ya makanisa wana masharti ambayo inabidi uyafuate lakini hawakuambii kwamba imani katika Kristo ndiyo ambayo kwa kweli inaokoa, wala hawaangalii kwamba mtu amefanya uamuzi huo wa kuamini. Watu wengine wanaweza kudai kuwa wanaamini lakini ukweli ni kwamba ni waigizaji tu, ni wanafiki. Katika kanisa letu, huwa tunawataka watu wanaotaka kujiunga na kanisa letu watoe ushuhuda wao kuwa ni lini walifanya uamuzi wa kumpokea Kristo kama Mwokozi wao. Lakini hata kwa hilo bado tunaweza kudanganywa. Ni Mungu tu ndiye anayeijua mioyo!

Ni Kwa Nini Kuna Madhehebu Mengi Ya Kikristo?

Madhehebu mengi yalianza kwa kukubaliana kuhusu mapokeo ya mafundisho fulani na kutokukubaliana katika mengine kama vile namna ya ubatizo, kama mtu anaweza kupoteza wokovu wake, namna za uponyaji wa kimwili, karama za kiroho na namna za kuabudu kanisani. Ninaamini kwamba aina nyingi za madhehebu tulizo nazo zinakidhi mahitaji ya watu wa aina mbalimbali. Kuna wanaopenda liturgia ya namna fulani, kuna wanaopenda mafundisho ya ndani sana ya Biblia, kuna wanaopenda burudani, wengine wanapenda nyimbo za kuchangamka na kuamsha hisia na wengine ni kwa kiasi tu.

Uongozi Wa Kanisa

Kuna aina tatu kuu za uongozi wa kanisa.

Uongozi wa ki-episkopo (Episcopos): Katika uongozi huu mamlaka ya kanisa hukaa katika Askofu. (Kwa Wamethodisti ni ule rahisi; ila kwa Waanglikana ni mgumu kidogo; na kwa Wakatoliki wa Rumi utawala upo kwa Papa)

Uongozi wa ki-presibiti (Presbuteros): Mamlaka ya kanisa ipo katika kundi la wawakilishi ambao wamepewa mamlaka na kusanyiko lote pamoja na wazee. (Hii ipo kwa kanisa la Presibiterian na makanisa mengine ya kiBiblia.)

Uongozi wa Kusanyiko: Huu ni uongozi unaosisitiza juu ya nafasi ya kila Mkristo mmoja-mmoja, jambo linalofanya kusanyiko liwe na uamuzi wa mwisho katika maamuzi. Kila mwamini ana kura ya maamuzi. (Hii ipo kwa makanisa ya ki-Baptisti na makanisa mengine ya Kiinjili, pia makanisa huru na ya kiBiblia.) Kanisa letu ni muunganiko wa hayo mawili ya mwisho. Tunaongozwa na wazee na kusimamiwa na mtu mmoja aliyeajiriwa, na kusanyiko huwa linapiga kura juu ya Mchungaji wanayemtaka. Mchungaji Msaidizi, Wazee, na bajeti.

Wazee Wa Kanisa

Uongozi wa Kiroho ni wajibu wa wazee. Sifa za wazee tunazipata katika 1 Timotheo 3:1-7 na Tito 1:6-9, ambapo kazi hii wamepewa wanaume. Wanao wajibu wa kulilinda kanisa dhidi ya mafundisho potofu na kulihudumia kanisa kama wachungaji wanaochunga kundi la Mungu. (Matendo 20:17, 28)

Mashemasi

Mashemasi wanafanya kazi ya uongozi katika mamlaka waliyo nayo wazee. Hawa huwa wanatunza washirika walio na mahitaji katika kanisa. Wanawake wanaweza kuwa mashemasi. (Warumi 16; 1 Timotheo 3:8-11.)

Taratibu Za Kanisa La Mahali

Taratibu:Ni mambo ya nje yaliyoelezewa na Kristo yanayofanywa na kanisa.”

Makanisa mengi huziita sakramenti.

Sakramenti: “Sakramenti ni kitu kinacholetwa kwenye milango ya fahamu kikiwa na nguvu, kwa uwezo wa kiungu, sio kwa ajili ya kuweka alama tu, lakini pia kikiwa na uwezo wa kuleta neema.” (Kwa mujibu wa Baraza la Katoliki).

Hatuamini kwamba ama Chakula cha Bwana au ubatizo ni namna ya kupeleka neema. Tunaamini kwamba vitu hivi hufanywa kwa kuyatii maagizo ya Kristo na kutoa taswira ya kile ambacho tayari kimeshafanyika ndani ya mioyo yetu. Matendo haya yote hukumbusha juu ya kufa, kuzikwa na kufufuka kwa Kristo.

Ubatizo

Soma: Mathayo 28:19

Namna: Kuzamisha ndiyo maana ya msingi ya neno ubatizo (baptize)

Kuzamisha hutoa picha ya umuhimu wa ubatizo, ambapo ni kifo cha mtu wa kale na kufufuliwa kwa mtu mpya. Kanisa hili linabatiza kwa kuzamisha, lakini linabishana na kugawanyika juu namna za kubatiza jambo ambalo halina tija. Kila mwamini anapaswa kubatizwa mara baada ya kujua kuwa Kristo aliagiza hivyo. Ni ushuhuda wa hadharani kwamba umeungana na Kristo. Kama ulibatizwa kabla ya kuamini, usisite kubatizwa tena kama mwamini. Ubatizo ni utii kwa Bwana wako.

Chakula Cha Bwana, Ushirika Au Ekaristi

Soma: 1 Wakorintho 11:23-32.

Kuna makusudi kadhaa ya kushiriki Chakula cha Bwana au Meza ya Bwana.

  1. Ni ukumbusho wa maisha na kifo cha Bwana wetu. Mkate usiotiwa chachu unawakilisha maisha makamilifu ya Bwana wetu ambayo yalimpa sifa ya kuwa sadaka inayokubalika kwa ajili ya dhambi zetu. Inawakilisha mwili wake ambao ulibeba dhambi zetu pale msalabani. Mvinyo unawakilisha damu yake aliyoimwaga kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu.
  2. 1 Wakorintho 11:26 inasema kwamba chakula hiki hutangaza mambo ya msingi ya injili. Hutangaza mauti ya Bwana.
  3. Ni kutukumbusha kwamba Yesu Kristo anarudi tena na tunapaswa kuendelea kushiriki hadi ajapo.
  4. Inapaswa itukumbushe kuhusu Umoja wetu sisi kwa sisi katika mwili wa Kristo na ushirika tunaoushiriki kama viungo katika mwili huo (1 Wakorintho 10:17).

Ni nani anayeweza kushiriki?

Mtu asiyeamini hapaswi kushiriki kwa sababu karamu hii ni utambulisho kwa hao ambao wamekiri imani katika kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo kwa ajili ya upatanisho wa dhambi zao.

Je, mwamini yeyote anaweza kushiriki bila kujali kuwa ni wa dhehebu gani? Jibu ni ndio. Hii ni Meza ya Bwana na waamini wote wa kanisa la ulimwengu wanaalikwa. Sio meza ya kanisa la kiBaptisti, kikatoliki au kipentekoste. Migawanyiko hii ni kinyume na wito wa watu wote kuwa wamoja katika kanisa la ulimwengu wote. (Uliofanyika Lausanne)

Onyo! 1 Wakorintho 11:27-32: Tunapaswa kuipeleleza mioyo yetu Na kuungama dhambi zetu kabla ya kushiriki Meza ya Bwana. Vinginevyo tunaweza kubadilishwa—Kama vile kugusa au hata kufa.

Kusudi La Kanisa La Mahali

  1. Kuabudu na kuonyesha upendo wake kwa Bwana (Ufunuo 2:4).
  2. Kuwahudumia waamini wake ili waweze kutiana moyo katika kupendana na kufanya matendo mema (Waebrania 10:24).
  3. Kushiriki katika kulitii Agizo Kuu. Yaani kwamba Injili ihubiriwe katika huduma za kanisa ili wasioamini waipokee na kuokoka.
  4. Kuwajali waamini wake ambao wana mahitaji, kama wajane, yatima na maskini (Yakobo 1:27; 1 Timotheo 5:1-16)
  5. Kufanya matendo mema katika ulimwengu (Wagalatia 6:10).
  6. Kuzalisha Wakristo waliokomaa, wenye msimamo na watakatifu (Wakolosai 1:28; Waebrania 6:1; Waefeso 4:14-16). Hii inaweza kumaanisha kuwa na nidhamu katika eneo la maadili na usafi katika mafundisho (1 Wakorintho 5, 2 Timotheo 2:16-18).

VIelelezo Vya Kanisa La Ulimwengu

Kristo ni Mchungaji na sisi ni kondoo (Yohana 10) – utunzaji na usalama

Kristo ni mzabibu na sisi ni matawi (Yohana 15) – kuzaa na kupata nguvu

Kristo ni jiwe la Pembeni na sisi ni mawe katika jengo (Waefeso 2:19-21) –Jiwe la pembeni hutoa mwelekeo na huwekwa mara moja tu.

Kristo ndiye Kuhani Mkuu na sisi ni ufalme wa makuhani (1 Petro 2) –tunajitoa kwake, nafsi zetu na huduma zetu.

Kristo ni Kichwa na sisi ni viungo vya mwili Wake (1 Wakorintho 12)—akiwa kama Kichwa, huongeza; na sisi kama viungo tunahudumiana kwa kutumia karama za kiroho ambazo ametugawia.

Kristo ni Bwana-Arusi na sisi ni bibi-arusi wake (Waefeso 5:25-33, Ufunuo 19:7-8)—upendo wa milele na ukaribu.

Kristo ni Mrithi na sisi ni warithi-wenzake (Waebrania 1:2, Warumi 1:17)—tutaushiriki utukufu wake.

Kristo ni Malimbuko na sisi ni mavuno (1 Wakorintho 15:23)—ufufuko wake unatuhakikishia kuwa na sisi tutafufuka.

Kristo ni Bwana na sisi ni watumishi Wake (Wakolosai 4:1, 1 Wakorintho 7:22)—mtumishi hufanya mapenzi ya bwana wake. Bwana naye humtunza mtumishi wake.

Sasa Tunayatendeaje Kazi Mambo Haya?

Inatupasa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa tunajiunga na kanisa la ulimwengu wote, bila kujali kuwa tunaabudu kwenye dhehebu gani. Kuwa katika kanisa la ulimwengu wote kunafanyika wakati mtu anapompokea Bwana Yesu Kristo kama Mwokozi wako. Kuna uhakika mkubwa sana katika kujua kwamba wewe ni miongoni mwa walioko katika kanisa la ulimwengu wote, yaani Mwili wa Kristo. Uhakika huu unatakiwa ukutie moyo kujitambulisha katika kanisa la mahali ambapo utaweza kukua na kutumika. Kanisa kama la kwetu halihitaji uwe mwanachama ili upate huduma zetu. Lakini huoni kwamba ni vizuri kuunga mkono na kutoa ufadhili mahali ambapo unapokea baraka na ukuaji wa kiroho kwa kujiunga kikamilifu? Kujiunga kikamilifu ni kujitambulisha na watu waliopo hapo. Hiyo ndio familia yako. Ndiko unakotoa sadaka zako kifedha. Ndipo pia utakaposaidia wale walio na mahitaji. Unafanya ushirika wako hapo, yaani UNAJITOA KIKAMILIFU! Kama umekuwa ukija kusali katika hilo kanisa kila Jumapili, kwa nini usiamue kulifanya kanisa lako na ujiunge kabisa? Madarasa ya waamini wapya hufanyika mara nne kwa mwaka. Huwa yanafanyika kwa Jumapili mbili mfululizo zinazofuatana asubuhi. Ukipenda kujiunga utaonana na mzee wa kanisa, atakuuliza maswali na kukuongoza ili uweze kutoa ushuhuda wako. Kisha utatambulishwa rasmi katika kanisa.

Maswali unayoulizwa yanahusu uelewa wako juu ya msimamo wa kanisa hili na kuhakikisha kuwa una msingi na rasilimali muhimu kwa ajili ya mtu yeyote atakayekuuliza kwamba, “Kanisa lako linaamini nini”?

Maswali Ya Kujifunza

Soma: Mathayo 16:13-18; Matendo 2:1-4, 41-47

1. Je, Yesu alitumia wakati gani kulizungumzia kanisa wakati alipokuwa hapa duniani? Je, kanisa lilizaliwa lini? Je, kuna shughuli gani zinazowatambulisha waamini katika kanisa?

Soma: 1 Wakorintho 3:9-10; Waefeso 2:19-22

2. Ni nani ambaye ndiye pekee msingi wa kanisa?

Soma: 1 Timotheo 3:15; 1 Wakorintho 12:13, 27; Waefeso 2:19-22; Waefeso 5:30-32

3. Katika kila aya uliyosoma, kanisa linaitwaje? Ni nini umuhimu wa kila alama? Je, unafikiri hii inaelezea kanisa la mahali au kanisa la ulimwengu? Ni nani washirika wa kanisa la ulimwengu wote? Je, wanatofautianaje na washirika wa kanisa la mahali?

Soma: 1 Wakorintho 12

4. Sura hii inakuambia nini kuhusu jinsi washirika wa mwili wa Kristo wanavyopaswa kutumika?

Soma Mathayo 26:26-29; Luka 22:19-20; 1 Wakorintho 11:23-31

5. Ni utaratibu upi ambao Yesu aliamuru kanisa Lake liutunze hadi arudipo? Je, unatukumbusha nini? Ni nini kinampasa kila mmoja wetu kukifanya kabla ya kushiriki? Ni adhabu gani itakayompata mtu atakayeshiriki “isivyostahili”?

Soma Mathayo 28:18-20; Matendo 2:36-47; Warumi 6:1-5

6. Ni utaratibu gani mwingine ambao Yesu aliamuru kanisa liutunze? Huu ulitunzwa lini kwa kanisa la mwanzo? Je, utaratibu huu ni alama ya nini? Je, unakuwaje ushuhuda kwa wengine?

Soma Yohana 15:9-10

7. Je, ni sababu ipi inayowafanya waamini wabatizwe na kushiriki ushirika wa meza ya Bwana? Je, utii wetu unathibitisha nini? Je umeshabatizwa tangu ulipomwamini Kristo?

8. Ni kwa nini ni muhimu kwamba tujishirikishe na kanisa la mahali kwa ajili ya ukuaji na ukomavu wetu kiroho? Je, ni nini tutakikosa kama tutakuwa tu washirika wa kanisa la mahali? Utamjibu nini mwamini anayesema, “Sihitaji kwenda kanisani. Ninamwabudu Mungu peke yangu”?

Related Topics: Curriculum, Ecclesiology (The Church)

Report Inappropriate Ad