MENU

Where the world comes to study the Bible

Kutafakari Uhakika wa Kimaandiko

Related Media

Utangulizi

Mungu amejifunua mwenyewe kwa njia nyingi za ajabu katika historia (Ebr. 1:1-4). Amejifunua katika asili (Zab. 19:1-6), lakini pia amejifunua kwa matendo yake katika ulimwengu. Hayo “matendo” ya Mungu kama mafuriko, kutoka utumwani, na pia kuonekana kwake katika maono, ndoto n.k. –yote haya yaliandikwa kwa ajili yetu katika Maandiko, ambayo ni “ufunuo” kutoka kwa Mungu. Sababu iliyomfanya Mungu ainue watu kadhaa waandike matendo yake ilikuwa ni ili baadaye vizazi vya watu wake, kwa msaada wa Roho wake waelewe kuwa Yeye ni nani, jinsi ya kuwa na ushirika Naye, na jinsi ya kuishi katika namna itakayompa heshima na kuleta furaha kubwa kabisa kwetu kama watu wake (2 Tim. 3:16-17).

Kwa kuwa neno la Mungu mara zote limekuwa muhimu kwa Wakristo—na ndivyo lilivyo na kwa kuwa linatupa picha ya wazi ya kuwa Mungu ni nani, inakuwa muhimu kwamba tujifunze jinsi ya kujilisha neno mara kwa mara katika nafsi zetu. Tukiwa na jambo hili, hapa kuna aya tano kutoka katika Maandiko zinazosisitiza hakika fulani ambazo sisi kama Wakristo tunazo. Hakika hizi ni muhimu kwetu kuzijua ili tuweze kukua na kuwa imara katika maisha ya Kikristo. Nilijifunza hakika hizi miaka mingi iliyopita nilipokuwa nafanya kazi baharini na tangu wakati huo zimekuwa zikinisahihisha, kunikemea, na kunitia moyo kwani ni kweli kuu sana. Ilikuwa ni katika aya hizi ndipo nilipojifunza kwa mara ya kwanza jinsi ya kutafakari Maandiko na nakushauri na wewe ujaribu kufanya hivyo pia.

Lakini tuna maana gani tunaposema “kutafakari”? hapa hatuzungumzii kumwaga kila kitu katika akili zetu tunachofikiri (jambo ambalo hata hivyo haliwezekani), lakini tuna maana ya kujaza akili yetu na neno la Mungu kwa kulifikiria kwa makini na kwa undani, huku tukimwomba Mungu atupe ufahamu katika jambo hili.

Hapa nina maswali kadhaa ambayo unaweza kujiuliza katika aya yoyote ili uweze kuingia ndani kwa kina na kupata uzima.

  1. Je kuna dhambi ya kuacha?:
  2. Je kuna ahadi ya kuidai?
  3. Je kuna mfano wa kuiga?
  4. Je kuna kosa la kuepuka?
  5. Je kuna jambo jipya kuhusu Kristo au Roho Mtakatifu?

Jaribu kukumbuka maneno haya kwa njia rahisi jinsi utakavyoweza na pengine maswali yafuatayo hapa chini Yanaweza kukusaidia zaidi:

  1. Ni jambo gani ambalo nililipenda au sikulipenda katika aya hii?
  2. Aya hii inanifundisha nini kuhusu Mungu?
  3. Aya hii inanifundisha nini kuhusu mimi mwenyewe na wengine?
  4. Je, kuna lolote katika aya hii nisilolielewa na ningehitaji ufafanuzi?
  5. Mungu anasema nini na mimi kuhusu aya hii?

Hapa kuna maswali mengine,

  1. Aya hii inanifundisha nini mimi kuhusu Mungu?
  2. Aya hii inanifundisha nini kuhusu mimi na mahusiano?
  3. Aya hii inanifundisha nini kuhusu wokovu na kumwishia Mungu?
  4. Aya hii inanifundisha nini kuhusu vita ya kiroho?

Wakati wa kutafakari na kujiuliza maswali haya, watu wengi wamegundua kwamba inasaidia sana kukariri aya kisha kutafakari juu ya kila neno lililoko kwenye aya husika. Kwa mfano, katika Wagalatia 2:20, Paulo anasema,

Nimesulubiwa pamoja na Kristo ila si mimi ninayeishi, bali ni Kristo anaishi ndani yangu. Kwa hiyo uhai nilio nao katika mwili, ni kwa sababu ya uaminifu wa Mwana wa Mungu, aliyenipenda akayatoa maisha yake kwa ajili yangu.

Namna ya kuanza kutafakari mstari huu, baada ya kuisoma aya na muktadha wake mara kadhaa, ni kusisitiza kila neno ili uweze kupata ujumbe katika hiyo aya mara kadhaa. Kisha, katika hali ya maombi fupisha hiyo aya kwa maneno yako mwenyewe na kumwomba Mungu akupe ufunuo juu ya umuhimu wake kwako na kwa wengine. Hakikisha ufupisho wako unakubaliana na mstari huo katika muktadha wake. Hili linawezekana pia kwa kusoma ule muktadha tena kwa kulinganisha na aya nyingine za Paulo na zilizoko katika Biblia.

Ukishafanya haya na hakika zinazofuata, unaweza kumsaidia mtu mwingine kutafakari pia. Katika mazungumzo yanayofuata nitaorodhesha mstari unaohusiana na uhakika na kisha kukushirikisha tafakari fupi na rahisi katika aya husika. Lengo hapa ni kumtia moyo mwamini mpya.

Masomo kuhusu Uhakika

Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu kuwa sisi tu wana wa Mungu (Rum. 8:16)

Uhakika wa Wokovu – 1 Yoh 5:11-12

4Na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu. Mwenye kushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu bali katika maji na katika damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli. Kwa maana wako watatu washuhudiao, Roho na maji na damu, na hawa watatu hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa watu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa maana huu ndio ushuhuda wa Mungu kwamba amemshuhudia Mwanawe. [Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe.] Na huu ndio ushuhuda kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Aliye naye Mwana anao huo uzima, asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo haya, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini jina la Mwana wa Mungu.

Mazingira: Yohana aliandika waraka huu kukabiliana na walimu wa uongo ambao walifundisha kwamba Kristo hakuwa mwanadamu kweli, lakini alionekana tu hivyo. Tatizo hapa ni kwamba, kama hakuwa kweli mwanadamu asingeweza kufa kwa ajili ya dhambi zetu, yaani, kufa kwa ajili yetu. Lakini ubatizo (maji) wake na kifo (damu yake) pamoja na Roho Mtakatifu—hawa wote wanaonyesha kuwa alikuwa mwanadamu kweli (na Mungu kweli) na kwamba alikufa kwa ajili ya dhambi zetu.

Mafundisho: Yohana ana uhakika juu ya uzima wa milele kwa ajili yetu; hana wasiwasi wala mashaka na anasema kwamba huu ni ushuhuda wa Mungu mwenyewe. Angalia hapa kwamba ni uzima ambao Mungu ametupa na kwamba uzima huu unahusu kuwa na Yesu moyoni. Hakuna eneo la katikati. Ni ama mtu awe na Mwana ili awe na uzima au mtu asiwe na Mwana na akose uzima. Tunapaswa pia kukumbuka kwamba uzima unapokelewa kwa kuamini na sio kwa matendo mema (Warumi 4:1-8; Waefeso 2:8-9). Mwisho, angalia uhusiano kati ya Yohana kuwaandikia na wao kujua kuwa wana uzima wa milele (mst. 13): kwa ajili yetu, tunapaswa kukumbuka kwamba uhakika wa wokovu huja kimsingi kupitia katika kumsikiliza Mungu katika Maandiko kwa jinsi Roho wake anavyoweka neno lake katika mioyo yetu.

Uhakika wa Msamaha—1Yohana 1:9

1:5 Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lolote hamna ndani yake. 1:6Tukisema kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli. 1:7Bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. 1:8Tukisema kwamba hatuna hatia ya dhambi, tunajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani mwetu. 1:9Lakini tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. 1:10Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo ndani mwetu. 2:1(Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi.) Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, 2:2naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.

Mazingira: Kuna uhusiano gani kati ya madai yetu kuwa tunamjua Mungu na jinsi tunavyoishi? Ni nini tunachokifanya tunapotenda dhambi? Haya ni baadhi tu ya maswali ya msingi ambayo Yohana alikuwa akijaribu kuyajibu hapa katika 1 Yohana 1:5-2:2

Mafundisho: Yohana anaposema kuwa Mungu ni nuru, hapa anaangazia usafi wa Mungu wa maadili na utakatifu. Sisi kama Wakristo tunapaswa kulielewa hili ili tuweze kufahamu uhusiano uliopo kati ya kudai kuwa tunamjua Mungu na jinsi tunavyoishi. Kwa bahati mbaya, utamaduni wa kizazi kipya ambao tunaishi hauoni uhusiano hasa kati ya hali ya kiroho na namna tunavyoishi ambapo upendo ndicho kipimo. Wakati fulani nilikuwa na mwanamke fulani katika kikundi chetu cha kujifunza Biblia ambaye alitangaza kuwa anamjua Kristo, lakini aliendelea kufanya zinaa na dhambi zingine. Huenda alitudanganya kwa kitambo, ingawa baadaye tulimgundua, lakini kwa hakika hakumdanganya Bwana. Kwa maisha yake alidanganya kwa kile alichokuwa akikisema. Tunapaswa kutambua kwamba, kama tunamjua Mungu, tutaonyesha ushahidi wake katika maisha yetu. Kwa upande mwingine, kama tunadai kuwa tunamjua Mungu halafu tunaishi kama Shetani, hapa tena tunadangaya kile tunachokisema. Kristo ndiye mfano wa utakatifu ambao tunapaswa kufuata.

Jambo jingine tunaloliona katika 1 Yoh. 1:5-2:2 ni kwamba hakuna mahali katika maisha haya ya Kikristo ambapo kuna ukamilifu kabisa. Mtu yeyote anayedai kuwa mkamilifu bila dhambi yoyote, Yohana anatuambia kuwa anajidanganya, na hana kweli ndani yake na anapotosha ukweli wa Mungu. Hakuna mtu miongoni mwetu atakayekuwa mkamilifu hadi tutakapotukuzwa (linganisha na 1 Yoh. 3:2-3). Kwa kweli hata tunapokuwa katika ushirika wa sisi kwa sisi, bado tunaihitaji damu ya Yesu (Roho anatumia manufaa ya kifo cha Yesu) ili kuondoa dhambi zetu.

Kwa hiyo sisi kama Wakristo, tunaishi katika changamoto ya kutaka kumpendeza Mungu na mara nyingine kumhuzunisha tunapotenda dhambi. Hivi tunaishije ili kukabili dhambi yetu? Je huwa tunatafuta vitabu kwa ajili ya msaada binafsi? Je tatizo letu ni kukosa maarifa tu? Je tunajificha chini ya mkeka? Au tunasema, “Ah, mimi ndivyo nilivyo tu?” au “Wakati ule nilibanwa, n.k.”? Yohana anasema tunapaswa kuziungama dhambi zetu, yaani, tuziungame dhambi zile ambazo hazionyeshi kuwa tunahusiana vizuri na Mungu “ambaye ni nuru” na ambaye ndani yake “hakuna giza.”

Yohana pia anasema anawaandikia watu wa Mungu ili kwamba wasitende dhambi (2:1). Hapa tena kuna uhusiano kati ya neno la Mungu lililoandikwa na maisha ya kiroho na ukuaji wa Wakristo. Hili ni lazima tulikumbuke. Waraka huu usingewafaa wasomaji wake, yaani, Roho hangeweza kuutumia kama njia ya neema, kama wangeshindwa kusoma, kuutafakari kwa makini, kuelewa, na kuutendea kazi.

Angalia kinachotokea tunapoungama dhambi zetu: zinasamehewa na sisi tunatakaswa, yaani, dhamiri na fikra zetu zinatakaswa na kuwekwa huru. Hii ndiyo namna ya kushughulikia dhambi zetu na hii ndiyo namna ambayo Mungu hufanya sisi tunapofanya sehemu yetu.

Mwisho, mara zote husianisha msamaha na kila manufaa ya kiroho kwa Kristo na kazi yake msalabani. Yohana amefanya hivyo na sisi tunapaswa kufanya hivyo. Tuko katika uhusiano ambao umejengwa katika neema ya Mungu na sio nguvu zetu.

Uhakika wa Maombi Yaliyojibiwa—Yohana 16:24

16:19Yesu aliweza kuona kwamba walitaka kumuuliza juu ya mambo haya, akawaambia, “Ndilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?” 16:20Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 16:21Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. 16:22Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye. 16:23Tena siku ile hamtauliza neno lolote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. 16:24Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; Ombeni nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. 16:25 “Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambapo sitasema nanyi tena kwa Mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. 16:26Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; 16:27kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba. 16:28Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.” 16:29Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yoyote! 16:30Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu.”

Mazingira: Yesu anakwenda kwa Baba, yaani, wakati wa kutukuzwa kwake kwa njia ya kufa, kufufuka na kupaa umewadia. Atawaacha wanafunzi. Hata hivyo, anawahakikishia wanafunzi wake juu ya uwepo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye baadaye angemtuma kwao (linganisha Yohana 14:26; 15:26; 16:13-14; Matendo 2). Hata hivyo, wanafunzi wana maswali mengi ya kumwuliza. Lakini anawaambia kwamba wanaweza kuuliza kwa jina lake, yaani kwa msingi wa mamlaka na uhusiano wake na Baba. Kwa maneno mengine, wamempenda Mwana wa Baba kiasi kwamba wanaweza kwenda kwa Baba kupitia Mwanawe na Baba atayapokea. Wanaweza kumwomba Baba kwa jina la Mwana, na Baba atajibu maombi yao.

Mafundisho: Angalia mambo matatu kuhusu maombi katika Yn. 16:24. Kwanza, kuna uhakika kwamba tukienda kupitia kwa Mwana (kwa kutambua kuwa yeye ni nani na nafasi yake) tutapokea (I Yoh. 5:14-15). Pili, kutakuwa na furaha kuu inayoambatana na Mungu kujibu maombi yetu, hasa yale maombi yanayoomba kumjua Mungu vizuri zaidi. Tatu, kama Wakristo tunapaswa kutambua kwamba tunakuja kwa Baba, kupitia kwa Mwana, kwa nguvu ya Roho. Maombi ni njia kuu ya kuhusiana na Utatu wa Mungu.

Uhakika wa Kuongozwa—Mithali 3:5-6

3:5Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; 6katika njia zako zote mkiri yeye, naye atanyoosha mapito yako.

Mazingira: Hakuna mazingira ya ajabu sana katika Mithali 3:5-6 ingawa Mithali 3:1-12 inasisitiza kweli na unyenyekevu, pamoja na kumtumaini na kumheshimu Mungu. Sehemu hii (Mithali 3:1-12) ni sehemu ya kifungu kikubwa zaidi cha Mithali 1 hadi 9., ambapo hekima hudhihirishwa na kuishi katika maadili safi na utauwa, kwa upande mmoja, na kujihadhari na mambo kama uzinzi, tamaa, maisha machafu kwa upande mwingine. Mithali ni misemo “yenye hekima” ambayo kwa kawaida huwa ni kweli. Misemo mingine husema moja kwa moja kile kilicho kweli kabisa ilhali zilizo nyingi husema kile kilicho kweli katika mahusiano ya kibinadamu. Kwa sehemu kubwa hazichukuliwi kuwa kauli za dhati, isipokuwa pale tu ambapo imeelezwa hivyo. Kwa mfano, Mithali 12:24, “Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.” Hii kwa jumla ni kweli, lakini sio kwamba ni kweli mara zote. Kuna watu wavivu wanawekwa kwenye utawala na wengine wenye bidii wanatawaliwa na watu wavivu.

Hata hivyo, katika Mithali 3:5-6 mkazo uko katika kumtumaini Mungu na ahadi ni kwamba “atanyoosha mapito yako”. Kama tukichukulia kwamba “atanyoosha mapito yangu” ina maana kwamba Mungu atanipa maisha makamilifu ambayo sitakaa nikutane na mambo magumu, basi hii itakuwa sio sawa; hata hivyo, kwa kusema ukweli, itakuwa sio tafsiri sahihi. Lakini tukielewa kwamba, “atanyoosha mapito yangu” ina maana ya, “atakuongoza kwenye maisha yanayompendeza, kwenye maadili na tabia njema,” basi hii Mithali itakuwa ni sawa. Mungu mara zote atafanya hivi kwa wale wanaoweka tumaini lao kwake kabisa.

Kwa hiyo ngoja nisisitize mambo machache kutoka katika Mithali hii. Kwanza, kumtumaini Mungu ni jambo la msingi katika kuwaongoza watu ambalo Mungu huwapa watu wake. Tunapaswa kudhamiria kumtumaini Mungu kwa ajili ya kupata uongozi wake, kwamba tunataka au la. Hata hivyo, yeye ndiye Mwenye mipango yote. Pili, hatupaswi kumwamini kwa sehemu tu ya moyo, lakini kwa moyo wetu wote, yaani, kwa nguvu zetu zote! Mungu hatatoa uongozi kwa watu wanaocheza-cheza naye.

Tatu, Tumeambiwa “tusizitegemee akili zetu wenyewe.” Watu wengine hufikiri kwamba hii ina maana kwamba Wakristo hawatakiwi kufikiri, ili wasizitegemee akili zao. Sio hivyo kabisa! (Watu hao wanasahau kwamba ni Bwana aliyewapa hizo akili!) Anachomaanisha Sulemani hapa ni kwamba tusizitegemee akili za kibinadamu na uelewa wenye dhambi wa jinsi ya kuishi, yaani hali ya kutokuamini, kana kwamba Mungu hayupo. Akili zetu wenyewe zinasema, “unastahili hiki na kile,” “una haki zako,” “dai haki yako upewe,” “ni sawa kumdanganya mkeo,” “fursa haiji mara mbili, kwa hiyo anayetokea tu, nenda naye, usizubae n.k.” La hasha, hatupaswi kuzitegemea akili zinazofikiri kwa namna hiyo, bali tuzitegemee amri, maagizo na hekima ya Mungu. Tunajua kwamba Kristo alifanyika mtumishi na akafa kwa ajili yetu (Mk. 10:45), kwa hiyo sisi nasi tunapaswa kuyatoa maisha yetu (kwa hekima) kwa ajili ya wengine. Hii ndiyo maana ya kusema “katika njia zako zote mkiri.” Kumkiri Mungu katika njia zetu zote ni kinyume na kuzitegemea akili zetu wenyewe; inahusisha kumtii Mungu katika maeneo yote ya maisha yetu. Hii ndio sababu inahusisha kumtumaini Mungu kabisa.

Uhakika wa Msaada katka Majaribu—1 Wakorintho 10:13

10:1Kwa maana ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; 10:2wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; 10:3wote wakala chakula kilekile cha roho; 10:4wote wakanywa kinywaji kilekile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. 10:5Lakini wengi sana katika wao Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. 10:6Basi mambo hayo yalikuwa ni mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. 10:7Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, “Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.10:8Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. 10:9Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. 10:10Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu. 10:11Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. 10:12Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. 10:13Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mwezi kustahimili.

Mazingira: Wakorintho walikuwa ni kanisa lililokuwa limesheheni nguvu za kiroho, mamlaka na uhuru binafsi. Kwa kweli waling’aa waliangalia haki zao, kiasi kwamba walikuwa wakiutumia uhuru wa Mkristo wa kweli kiasi kwamba walikuwa wakileta huzuni kubwa kwa Wakristo wengine na kuhatarisha maisha yao ya kiroho pia. Baadhi ya Wakristo walikuwa wakila katika mahekalu ya sanamu kwa kuwa walijua kuwa kitu kama sanamu hakikuwepo. Lakini Paulo anawaambia, kwanza kabisa wako kwenye hatari ya kumkasirisha Bwana, na pili, wanajeruhi dhamiri za Wakristo wengine ambao wanaongozwa kwenda kwenye mahekalu ya sanamu kula lakini hawaelewi kitu (yaani, hakuna kitu kama sanamu) kama jinsi wao wanavyofanya.

Aya hii inaanzia 8:1 na inaenda hadi mwishoni mwa 10:33. Jambo analolisema Paulo hapa ni kwamba uhuru ni mzuri kama ukiongozwa na upendo, lakini unaharibu watu wanaodai kuwa wako huru na wengine kwa kuwa hufanyika katika ubinafsi. Tatizo hapa ni kwamba tunajaribiwa kufanya mambo kwa namna zetu na sio kwa namna ya Mungu. Hatupaswi kufikiri hata mara moja kwamba kwa kuwa tumeokoka basi tunaweza kutenda dhambi (kwa kisingizio cha kuwa huru) na dhambi isikae. Ingawa hatupotezi karama ya Mungu ya uzima wa milele, tunaweza kuyaharibu kabisa maisha yetu (na ya wengine pia). Tunapaswa kukumbuka kwamba tunapojaribiwa, Mungu hufanya mlango wa kutokea, lakini hii haina maana kwamba atatusaidia tu hata pale tunapojiingiza kwenye dhambi kwa makusudi kwa kujua.

Mafundisho: Katika I Wakorintho 10:1-4 Paulo anawakumbukusha mambo mazuri Waisraeli waliyoyapata. Sisi kama Wakristo pia tuna mambo yetu mazuri. Katika I Wakorintho 10:5-10, licha ya hayo mambo mazuri ya Waisraeli, Paulo anawakumbusha jambo Mungu alilofanya kutokana na uasi wao kule jangwani. Matokeo yake yalikuwa mabaya sana. Kisha katika 10:11-12, Paulo anawaambia hawa Wakristo wakaidi kwamba kilichowatokea Israeli ni mfano kwa Wakristo na kichukuliwe hivyo. Kwa kifupi Wakorintho walionywa kwa upendo na ukali pia na, kwa kweli ndivyo wengi walivyo leo. Tusimchukulie Mungu kama “kitu chepesi tu.” Tunapaswa kuwa na heshima kuu kwa ajili ya utakatifu na kujitunza, katika namna ya Kikristo. Sasa ni katika mazingira haya Paulo anazungumza kuhusu majaribu katika 10:13.

Mawazo mengi hujitokeza tunavyopitia kifungu hiki cha 1 Wakorintho 10:13. Kwanza jambo hili linakutana na uzoefu wetu juu ya majaribu kwa nyakati fulanifulani. Huwa inatokea kwa ghafla na inauma. Lakini tunapaswa kutambua kwamba haya majaribu huwa ni “ya kawaida” kama yalivyo kwa wanadamu walioanguka kwa ujumla. Hii haina maana kwamba kila mtu anakabiliwa na majaribu ya aina moja, lakini ni kwamba majaribu huwa ni ya kawaida kwa mwanadamu katika hali yake ya kuanguka katikati ya ulimwengu ulioanguka. Hii ina maana kwamba haya majaribu, pamoja na msaada wenye uaminifu wa Mungu yanaweza kushindwa. Hata hivyo, kutarajia msaada wa Mungu na huku unafanya dhambi na uovu kwa makusudi, kama vile kula chakula katika hekalu la masanamu, ni suala jingine gumu. Kama walivyokuwa wale Waisraeli waliotutangulia, kama tukijihusisha na dhambi hiyo, tunaweza kutarajia adhabu kali tu.

Paulo ni mwepesi kuweka wazi kwamba Mungu ni mwaminifu kutusaidia katika jaribu lolote, na pia anataja hapa namna ambayo Mungu hutuletea huo msaada, yaani kwa kutufanyia “mlango wa kutokea.” Neno hili la “kufanya mlango wa kutokea” ina maana ya “kumaliza hilo jaribu.” Kwa hiyo kuna kipindi maalum cha muda ambao majaribu ambayo Mungu anayaleta yatakaa kwa wakati wake, wakati huo akitusaidia kustahimili (yaani, Mungu ni mwaminifu). Majaribu haya yamekusudiwa yatufundishe kuishi katika namna ambayo itampa Mungu heshima (Yakobo 1:3-5).

Hitimisho

Kuna matumaini kwamba tafakari hizi zitawasukuma wengine kusoma Biblia, kuzitafakari kweli zake, na kupata msaada, maelekezo, ujasiri na maono kwa ajili ya kila siku. Kama umepitia aya hizi, na kujaribu kuziweka katika kumbukumbu, zitamsaidia mtu kufanya hivyo-hivyo. Biblia iliandikwa kwa ajili ya kutuelekeza: “Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na Tumaini”(Warumi 15:4).

Imeandikwa na Greg Herrick na kutafsiriwa kwa Kiswahili na Emmanuel Lyatuu

Greg Herrick anaishi Calgary Alberta, Canada pamoja na mkewe na watoto 4. Ana mzigo wa kufundisha na kulea wengine.

Ni Mchungaji na Ana shahada ya Th.M na PhD kutoka Dallas Theological Seminary

Related Topics: Assurance

Report Inappropriate Ad