MENU

Where the world comes to study the Bible

Report Inappropriate Ad

Kinachohitajika Ili Mtu Akue

Related Media

I. Ni Nini Kinahitajika Ili Mtu Akue Na Kukomaa? – Biblia

Tunaanza mfululizo mpya leo unaouliza swali: “Ni nini kinahitajika ili mtu akue?” Hii ni kama sehemu muhimu sana ya utafiti (ambapo unaweza kung’oa mmea na kukung’uta udongo wote kwenye mizizi na kuuweka mezani). Hapo lengo ni kuona kama ni kweli mmea unahitaji maji na udongo ili kukua au kama ni dhana tu inayoaminiwa na watu duniani.

A. Kusudi La Mfululizo Huu:

Kusudi ni lengo lilelile alilokuwa nalo Epafra kwa ajili ya Wakristo wa Kanisa la Kolosai. Aliwaombea,

“ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.” Wakolosai 4:12

Hilo ndilo Mungu analolitaka kwetu. Anataka kwamba sisi tukue na kuthibitika. Unaweza kuchorea mstari hayo maneno ya “kuthibitika” na “Mapenzi ya Mungu”. Yote hayo yameandikwa katika hili neno. Ni mapenzi ya Mungu kwamba tukue.

Sikiliza mstari huu kutoka kwa mtume Paulo:

Waefeso 4:14-15 “ili tusiwe tena watoto wachanga, …bali tukue hata tumfikie yeye aliye kichwa Kristo.”

Je uliwahi kutambua kuwa Mungu anakutaka ukue? Nina rafiki yangu ambaye anafanya kazi katika Kituo cha Afya kwa ajili ya walemavu wa akili. Siku moja nilikwenda naye hapo kituoni na nikawaona watu wa kiume na wa kike ambao wamekomaa miili yao lakini akili zao zilikuwa hazijakomaa. Ilikuwa ni shida! Kuna kijana mmoja ambaye alionekana kama alikuwa na miaka 20 akiwa katika kiti-mwendo. Msaidizi wake alikuwa akijaribu kuweka mpira mapajani mwake lakini yeye aliupiga kwa mikono yake ili utoke. Wakati mwingine ilimchukua dakika nzima kufanya hivyo. Wakati mwingine hata dakika 3 au 4.

Kama tukiuangalia ukuaji uliochelewa kiakili na kimwili tunaushangaa na kusema, “Ni shida!” Je, Mungu Baba atakuwa anatufikiriaje anapotuangalia na kuona na sisi tulivyochelewa kukua kiroho? Hapa sasa nikuulize swali…

B. Je, Ukomavu Wa Kiroho Ni Nini? Kuwa Kama Kristo!

Waefeso 4:13 hata na sisi sote tutakapoufikia Umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.

Kwa jinsi huu mstari ulivyo, unaweza kuuelezea ukomavu wa kiroho kwa sentensi moja: Ukomavu wa kiroho ni kuwa kama Kristo.

Wengi wetu tunataka kukua. Wengi wetu tunataka kukomaa. Wengi wetu tunataka kuwa kama Kristo. Mara nyingi hatujui namna ya kuanza.

C. Mapitio: Tabia Saba Za Wakristo Wanaokomaa

Tutajikita katika kuangalia Tabia Saba za Msingi ambazo kila Mkristo anahitaji kuwa nazo ili aweze kukua hadi kufikia ukomavu wa kiroho. Lengo langu ni …

Kukuwezesha kupata stadi au maarifa unayoyahitaji kwa ajili ya tabia hizi.

Kueleza vitu unavyovihitaji ili kuendeleza tabia hizi.

  1. Ili ukue unahitaji kula—Biblia
  2. Ili ukue unahitaji kupumua—Maombi
  3. Ili ukue unahitaji usafi wa kiroho—Kuungama dhambi
  4. Ili ukue unahitaji familia inayojali—Ushirika
  5. Ili ukue unahitaji mazoezi ya mara kwa mara—Huduma
  6. Ili ukue unahitaji ulinzi—Majaribu
  7. Ili ukue unahitaji kutoa—Uwakili

D. Kweli Juu Ya Ukuaji Wa Kiroho

1. Kukua Kiroho Hakutokei Tu Otomatiki.

Je, umewahi kujua kwamba unaweza kuwa Mkristo na ukashindwa kukua kiroho?

Waebrania 5:12-13 “Mmekuwa Wakristo kwa muda mrefu sasa, na mlipaswa kuwa mnafundisha wengine. Lakini badala yake mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu. Mmekuwa kama watoto wachanga ambao wanahitaji maziwa na hawawezi kula chakula kigumu. 13Mtu anayeishi kwa maziwa hajui sana neno la haki, kwa maana ni mtoto mchanga” (imetafsiriwa).

Huu ni ukuaji uliodumazwa. Hawa wanapaswa kukomaa. Walikuwa na muda wa kutosha. Lakini ni shida sasa kwamba hawajakomaa! Ukomavu hauji wenyewe. Unahitaji muda, kujibidisha na kadhalika.

2. Ukomavu Wa Kiroho Hautokei Kwa Haraka

Biblia inasema katika 2 Petro 3:18, “Lakini kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo.” Hapa inaonyesha kwamba ni mchakato. Inachukua muda. Sio jambo la mara moja.

Je unakumbuka zile hisabati za shuleni kwamba Mwendo x Muda = Umbali?

Hii kanuni ina maana kwamba ukisafiri kwa mwendo wa kilometa 5 kwa saa kwa masaa 100 utasafiri umbali wa kilometa 500

Ukisafiri kwa mwendo wa kilometa 50 kwa saa, kwa masaa 10 utasafiri umbali wa kilometa 500

Ukisafiri kwa mwendo wa kilometa 500 kwa saa, kwa masaa 10 utasafiri umbali wa kilometa 500

Kuna Wakristo ambao wamemfahamu Kristo kwa miaka 50. Kwa sasa walipaswa kuwa wamekomaa. Lakini ndio hao wanaenda kwa mwendo wa kilometa 1 kwa saa. Wengine hata hizo kilometa hazipo! Wamesimama tu, hawaendi popote. Wameketi tu, wanazuia wengine kusonga mbele maana wanasababisha msongamano nyuma yao.

Mstari wetu Mkuu: 2 Petro 3:18, “Lakini kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele! Amina”

Hakuna njia ya mkato ya kukua kiroho. Hakuna kidonge au dawa ambayo ningeweza kukupa ili ukishainywa leo na kesho uwe umekomaa kiroho. Ni jambo linalochukua muda. Linahitaji juhudi za makusudi. Haliji lenyewe wala haliji haraka.

Watu hujaribu njia nyingi za mkato. Wengine hutafuta tu kuhamasisha hisia zao—“Nikipata kitu hiki ‘fulani’ matatizo yangu yote yanakwisha na nitakuwa Mkristo aliyekomaa.” Watu wengine husema, “Nikihudhuria semina hii…Nikisoma kitabu hiki…Nikisikiliza kanda hii…” Watu wengine husema, “Nikifuata kanuni hizi, basi nitakuwa kama Mungu anavyonitaka niwe.”

Lakini Biblia inasema, hapana. Ni mchakato endelevu. Ni lazima ujifunze ili ukomae. Lakini kuna maarifa ambayo unatakiwa ujifunze ili uweze kukua.

3. Ukomavu Wa Kiroho Hauji Bila Nidhamu Binafsi

1 Timotheo 4:7 “Jitahidi na chukua muda kupata utauwa”(imetafsiriwa).

Je uimara wa kimwili hutokea wenyewe? Hapana. Ndivyo ilivyo hata kwa mazoezi ya nguvu za mwili. Inachukua muda na kufanya kazi. Ndivyo ilivyo kwa masuala ya kiroho, kuna mazoezi yanayohitajika kukujengea tabia za msingi katika maisha ya kiroho. Biblia inasema, “Jibidishe kwa lengo la kupata utauwa.” Kujibidisha hapa ndio kujenga nidhamu binafsi.

Unapozungumzia nidhamu binafsi unahitaji kuzungumzia pia ufuasi kwa sababu haya mawili yanakwenda pamoja. Kuna kweli sita za msingi ambazo nakutaka uzielewe kupata picha ya huko tunakoelekea.

1. Biblia inafundisha kuwa waamini waliokomaa wanaitwa wanafunzi. Hilo ni neno Biblia inalotumia kuelezea mwamini aliyekomaa—mwanafunzi.

2. Biblia inafundisha kuwa siwezi kuwa mwanafunzi bila kujenga nidhamu. Maneno haya mawili huwa yanaenda pamoja—mwanafunzi na nidhamu.

3. Biblia pia inafundisha kwamba kwa jinsi ninavyojengewa nidhamu ndivyo Mungu anavyoweza kunitumia.

4. Alama ya mwanafunzi ni kubeba msalaba.

Luka 14:27, Yesu alisema, “Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” Mungu anatutaka tubebe msalaba wetu. Tutaelezea maana ya maneno haya.

5. Haya mambo ninatakiwa niyafanye mara ngapi? Biblia inasema kila siku.

Luka 9:23 Akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.”

Hili ndilo tutakalokwenda kulizungumzia. Katika hali ya vitendo kubeba msalaba ina maana gani?

6. Hivi kubeba msalaba kunahusisha nini hasa? Imeshaelezwa: inahusisha jambo lolote linalompa Kristo nafasi ya kwanza katika maisha yangu.

E. Lengo: Kudhamiria Kuwa Na Tabia Zinazohitajika Kukomaa Kiroho

II. Sababu Zinazokufanya Uihitaji Biblia Yako.

A. Biblia Ni Kama Kitabu Cha Maelekezo Cha Mmiliki Wa Gari. Bila Hicho Maisha Yatakuwa Magumu Sana.

Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. 2 Timotheo 3:16-17

Kama una gari jipya, miongoni mwa mambo utakayofanya ni kusoma kitabu cha maelekezo. Utaangalia magurudumu kama yameisha. Utakagua mafuta (oili) kama yanahitaji kubadilishwa na utaangalia kama gari inahitaji kufanyiwa huduma mara ngapi. Unaangalia pia kwamba uende mwendo gani katika kilometa 200 za mwanzo. Ukishindwa kufanya haya yote, utaiharibu injini na kuua gari lako.

Mungu huwa anajali sana na hakututupa tu huku duniani na kusema, “Fanya vizuri kwa jinsi utakavyoweza! Natumaini kuwa utagundua kila kitu! Nakutakia kila la heri!”

Alitupatia kitabu cha maelekezo ya mtumiaji. Kitabu hicho kinatuambia kila kitu tunachokihitaji kumhusu Yeye, kuhusu sisi, na kuhusu maisha. Lakini haitusaidii chochote hadi tumeisoma!! Soma kitabu cha Mungu cha maelekezo!

B. Biblia Ni Kama Tochi Kwa Ajili Ya Giza. Bila Hiyo Lazima Utajikwaa Na Kuumia, Au Kutangatanga Na Kupotea.

Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu. Zaburi 119:105

Wewe uko katika kambi mpya. Ni usiku wa manane. Unajisikia kujisaidia. Halafu unatokea mlango wa nyuma bila tochi, na kujigonga kwenye meza halafu unaanguka. Ndio kusema bila mwanga njiani utajikwaa na kuumia au utangetange na kupotea.

Maisha ndio kama hivyo. Unajisikia kama vile unajikwaa, unatangatanga. Unavurugwa. Mungu hakukusudia kuwa maisha yawe hivyo. Alitupatia tochi. Lakini tochi haiwezi kutusaidia kama hatuitumii! Washa tochi ya Mungu!

C. Biblia Ni Kama Silaha Kwa Askari. Bila Hiyo Utakamatwa Au Kuuawa.

Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu. Waefeso 6:17.

Nimekuwa nikifundisha masomo ya Biblia kwa miaka mingi. Mara nyingine unakutana na wanafunzi ambao wanapenda kujifunza wakiwa wamehamasika sana. Wakati mwingine unakutana na wanafunzi waliochoka wasiokuwa na hamu kabisa na wala hawazingatii unachowafundisha.

Mara nyingi nimewaza, “Hawa wanafunzi hawajui kwamba wako katika vita. Hawatambui kwamba kitabu hiki ndiyo silaha yao pekee. Hawajui kwamba wasipojifunza ndani yake, wakajifunza namna ya kuitumia, watakufa na kusahaulika. Watasomwa kwenye orodha ya majeruhi wa kesho, wakiwa katika hali mbaya sana.”

Tuko katika vita ya kiroho. Kama wewe ni Mkristo basi wewe ndio mlengwa. Na usipojua kutumia upanga wa Roho, yaani Neno la Mungu, utakufa! Mungu hajakusudia kuwa uuawe au uwe majeruhi. Mungu amekusudia kuwa wewe uwe mpiganaji mshindi, sio majeruhi. Mungu alikupa upanga, lakini hautafanya kazi wenyewe bila wewe kuutumia! Uwe basi mjuzi wa kutumia upanga wa Mungu!

D. Biblia Ni Kama Kioo Kwa Mtendaji. Bila Hiyo Hutajua Kuwa Wewe Ukoje Wala Hutabadilisha Matendo Yako.

Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. Yakobo 1:22-25

Kioo huwa kinafanya nini? Kinakuonyesha jinsi wewe ulivyo. Asubuhi ya leo nilikaa kwa muda mbele ya kioo. Wengine hufikiri, “Huo muda hautoshi!”

Katika aya hii Yakobo anaeleza kuwa ni mwanaume anayejiangalia na kuondoka huku akisahau jinsi alivyo. Mwanamke hawezi kufanya hivyo. Yeye atafanya kila njia ili arudishe uso wake katika utukufu wa mwanzo ambao Mungu alimuumba nao!

Kazi ya kioo ni kuonyesha hasa jinsi tunavyoonekana, ili tuweze kufanya mabadiliko yanayotakiwa. Kazi ya Biblia ni kutuonyesha jinsi hasa tulivyo ili kwamba, kwa msaada wa Mungu, tufanye mabadiliko yanayotakiwa.

Ni shida sana wakati kila mtu anajua kuwa John anasengenya, lakini John mwenyewe halijui hilo. Ni shida pia wakati kila mtu anajua kuwa Betty ana ulimi wa mafarakano lakini Betty mwenyewe halijui hilo. Ni shida sana wakati kila mtu anajua kuwa Bosco anatumia pesa vibaya lakini Bosco mwenyewe halijui hilo.

Biblia ni kama kioo. Inaonyesha jinsi tulivyo. Inaonyesha mahali tunapohitaji kubadilika. Sio tu kuwa inatuonyesha hitaji, lakini pia inatusaidia kubadilika! Lakini kioo hakikusaidii chochote kama hukitumii! Jitazame katika kioo cha Mungu!

E. Biblia Ni Kama Virutubisho Na Maji Kwa Mmea. Bila Hivyo Utanyauka Na Kufa

Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki, wala hakusimama katika njia ya wakosaji wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji, uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alifanyalo litafanikiwa. Zaburi 1:1-3

Sasa turudi nyuma na kuangalia mawazo yangu hapa juu ya mmea. Halionekani kama jambo baya sana. Lakini kama nikiuacha mmea hapa hadi wiki ijayo, hivihivi bila maji na bila mbolea si unajua kitakachotokea? Mmea utakuwa umekufa na kuwa ni takataka.

Hii ndiyo shida. Kuna baadhi yenu mnaojaribu kuishi kwa namna hii. Kila Jumapili mnajaribu kupata chakula cha kiroho na maji mnayoyahitaji kwa wiki yote ijayo. Huwezi kufanya hivyo. Haiwezekani. Itakuwa kama huu mmea ambao unajaribu kuupa maji na virutubisho kwa saa moja tu kwa wiki. Sasa hii itasaidia nini kwa mmea huu? Hiyo itasaidia nini kwenye maisha yako ya kiroho? Hapa ndipo shida ilipo. Wengi wenu mnaufikiria mmea huu kuliko kufikiria juu ya maisha yenu ya kiroho. Mnajiwazia wenyewe, “Nafikiri huo mmea utaishi tu.”

Kama unaujali sana huu mmea, je, si zaidi sana ujali juu ya roho yako? Roho yako inahitaji maji yaliyoko katika Neno. Roho yako inahitaji chakula ambacho ni hiki Kitabu pekee kinaweza kukupa. Cha ajabu ni kwamba wewe unabaki kufa na njaa! Unakula mara moja kwa wiki, halafu unashangaa ni kwa nini maisha yako ya kiroho ni magumu! Unashangaa kwa nini unaendelea kuanguka katika dhambi. Unashangaa kwa nini maendeleo yako hayaonekani. Nitakueleza sababu—roho yako inakufa kwa njaa! Ningaliweza kukuandalia meza yenye vyakula vizuri sana unavyoweza kuwaza, lakini havitakusaidia kama hutakula! Sasa kula chakula cha Mungu!

Mathayo 4:2-4

2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.
3 Mjaribu akamjia akamwambia, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.”
4 Naye Yesu akajibu akasema, “Imeandikwa: ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’”

Kula chakula cha Mungu!

III. Hitimisho

Ningependa kukuhimiza kuchukua hatua nyingine ya kudhamiria kujifunza Neno la Mungu. Hapa kuna mambo yanayowezekana kuyafanya. Je uko tayari kuangalia mambo haya na kuchagua hapo moja ili ulifanye kwa mwaka huu?

A. Mapendekezo Kwa Ajili Ya Ukuaji Binafsi

1. Kwa Anayeanza

___Nitatumia mwongozo wa kusoma Biblia kila siku na Biblia yangu kwa siku_____kwa wiki.

___Nitasoma Biblia yangu dakika___kila siku, siku ___kwa wiki kwa mwaka huu.

___Nitasikiliza Biblia kwenye kaseti kwa dakika___kwa wiki mwaka huu.

___Nitakariri mistari___ya Maandiko kila wiki kwa mwaka huu.

___Nitanunua aina tofauti za Biblia na kuzitumia mwaka huu.

___Nitakuwa nikihudhuria masomo ya Biblia kila Jumapili kila saa tatu asubuhi.

___Nitajiunga na vikundi vya Kujifunza Biblia na kuwaomba wanisaidie kufikia malengo yangu ya kusoma Biblia mwaka huu.

2. Kwa Wanaoendelea

___Nitapanga kuhudhuria mafunzo ya kwenye mtandao mwezi Machi, na kufanyia mazoezi njia mpya za kujifunza Biblia mwaka huu.

___Nitasoma kitabu mwaka huu kuhusu jinsi ya kujifunza Biblia.

___Nitapunguza baadhi ya shughuli katika ratiba yangu ili nipate saa___ kwa wiki za kujifunza Biblia mwaka huu.

___Nitajifunza na kufanya mazoezi ya kutafakari Maandiko kwa dakika ___ kwa wiki mwaka huu.

___Nitajiandikisha kupata mafunzo juu ya kujifunza Biblia katika Umoja wa Kujisomea Biblia.

___Nitaandika malengo yangu ya kujifunza Biblia kwenye Kadi ndogo, kisha nimpatie rafiki yangu, na kumwomba anikumbushe na kuniuliza maendeleo yangu (Kwa mfano, “Lengo langu: Dakika 15 kwa siku, siku tano kwa wiki”)

3. Walioendelea

___Nitaandika mawazo ninayopata katika Biblia kwenye Daftari siku____ kwa wiki mwaka huu.

___Nitanunua na kutumia zana za kujifunza Biblia (kama Kamusi ya Biblia, Itifaki ya Biblia, Rejea Muhimu n.k.)

___Nitahudhuria vikundi vya kujifunza Biblia (Faragha, vikundi vya akina mama, Moms n.k. nijifunze nao Biblia mwaka huu.

___Nitanunua program ya Computer ya kujifunza Biblia kwa mwaka huu.

B. Mapendekezo Kwa Ajili Ya Ukuaji Wa Familia

___Tutafanya Mpango wa Familia wa kujifunza Biblia wiki hii.

___Tutaanza Maktaba ya Biblia kwa ajili ya Familia.

___Tutakariri kifungu cha Biblia pamoja kila wiki mwaka huu.

___Tutasoma kitabu kizima cha Biblia mwaka huu.

___Tutaulizana mara moja kwa wiki, “Umejifunza nini kwenye Biblia kwa wiki hii?

___Tutahudhuria Kambi ya Biblia kwa ajili ya Familia au Kongamano kwa Mwaka huu.

Na. John Underhill Imetafsiriwa kutoka Kiingereza na Mwl. Emmanuel Lyatuu

John Underhill ni Mchungaji katika Kanisa la South Hill Bible Church, lililoko Spokane, Washington, Marekani.

Related Topics: Basics for Christians, Bibliology (The Written Word)

Report Inappropriate Ad